Moshi. Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) Moshi kimeanza safari ya kuachana na nishati chafu na kuelekea matumizi ya nishati safi, hatua inayolenga kupunguza gharama za uendeshaji, kulinda afya za watumiaji na kuhifadhi mazingira.
“Kwa mujibu wa waraka wa Serikali wa kuhamasisha taasisi kuachana na nishati chafu, tumeanza kutumia majiko yanayochoma kuni mbadala (briquettes) na sasa tupo kwenye hatua ya kufunga mifumo ya gesi. Tayari tumeingia mkataba na Kampuni ya Taifa Gas kwa ajili ya usambazaji wa gesi na mitungi,” anasema.
Chuo hicho kinatumia majiko sita yanayochoma kuni mbadala, kikitumia tani tano kwa mwezi kwa gharama ya Sh600,000 kwa tani, hivyo hutumia Sh3 milioni kwa mwezi.
Kutokana na gharama kuwa kubwa, taasisi hiyo imejipanga kuharakisha mpango wa kuhamia kwenye matumizi ya gesi.
Veta Moshi yaanza kutumia nishati safi kupunguza gharama, muda na kulinda afya
Veta Moshi imekuwa ikijivunia kutengeneza majiko yake kupitia wanafunzi na walimu wa fani ya uchomeleaji, hatua inayopunguza gharama na kuongeza ujuzi wa vitendo.
Mwalimu wa uchomeleaji, Buruhani Rashid, anasema: “Ukitumia gesi ni nafuu zaidi kulinganisha na mkaa. Familia ya watu sita inaweza kutumia zaidi ya Sh120,000 kwa mwezi kwa mkaa, lakini kwa gesi ni karibu Sh52,000 pekee kwa mtungi wa kilo 15.”
Rashid anasema wametengeneza majiko zaidi ya 10 ya gesi na kuni mbadala kwa matumizi ya taasisi na familia. Pia wamehudumia taasisi saba tangu mwaka 2024.
Mpishi chuoni hapo, Saaduni Ally, anasema jikoni wanatumia mifuko saba ya briquettes yenye kilo 25 kila mmoja kwa siku ili kuandaa chakula cha wanafunzi.
“Afya yake si mbaya sana, ila gesi ni salama na nafuu zaidi, hasa tukizingatia uchafuzi wa mazingira,” anasema.
Serikali imekuwa ikihimiza taasisi kuhamia nishati safi kupitia Mpango wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034, ambao unalenga kufanikisha matumizi ya asilimia 80 ya nishati safi kwa kaya zote ifikapo mwaka 2034.
Habari hii imedhaminiwa na Taasisi ya Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.