TBA KUANZA OPARESHENI YA KUWATOA WADAIWA SUGU OKTOBA MOSI

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umetangaza kuanza oparesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu katika nyumba za Serikali kuanzia Oktoba 1, mwaka huu endapo watashindwa kulipa kodi zao za pango hadi Septemba 30.

Wito huo umetolewa leo Septemba 10, 2025 Jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua hiyo.

Arch. Daud Kandoro amesema wadaiwa wote wanapaswa kulipa kodi zao kulingana na mikataba yao kabla ya mwisho wa mwezi huu ili kuepuka kuondolewa kwa nguvu na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Hakutakuwa na muda wa ziada wa kulipa madeni. Wapangaji wote wanapaswa kulipa ndani ya muda uliopangwa,” amesema.

Aidha, amefafanua kuwa TBA ina utaratibu wa kisheria wa kuwapangisha watumishi wa umma na watu binafsi wenye sifa, na sasa inawataka wapangaji wasio na sifa kuzikabidhi nyumba hizo na kulipa malimbikizo ya kodi.

Amesema miongoni mwa wasiokuwa na sifa ni pamoja na watumishi waliopangiwa nyumba kisha kuhamia vituo vingine nje ya mkoa husika, waliostaafu kwa mujibu wa sheria, waliokufa na wale walioondoka kwenye utumishi wa umma.

Arch. Daud Kondoro ameongeza kuwa oparesheni hiyo itafanyika nchi nzima na hakuna atakayeachwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Miliki TBA, Said Mndeme, amesema taasisi hiyo inadai zaidi ya shilingi bilioni 4 kutoka kwa wapangaji ambao hawajalipa kodi ndani ya kipindi cha miezi mitatu na kuendelea.