DK.SAMIA ATAJA UPEKEE WA TABORA, ATAKA TANZANIA KUJITEGEMEA KIUCHUMI

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Tabora

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema mkoa wa Tabora una nafasi ya kipekee katika siasa nchini hasa uamuzi wa busara uliyosababisha nchi kuwa huru.

Amesema baada ya nchi kuwa na huru kisiasa sasa uliopatikana mwaka 1961 , mapambano yanayoendelea sasa ni ya uhuru wa kujitegemea kiuchumi.

Dk.Samia ameyasema hayo alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Tabaro ambapo amehitimisha kampeni za kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Katika Mkoa wa Tabora Dk.Samia amefanya mikutano ya kampeni katika Wilaya ya Igunga,Nzega,Uyui,Urambo ,Kaliua na kisha kihitimisha katika Manispaa ya Tabora Mjini kwa kuhutubia maelfu ya wananchi.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Nanenane Ipuli, Dk. Samia amesema Tabora ina nafasi ya kipekee katika historia ya kisiasa nchini.

“Mmoja wa waasisi na Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisoma katika mkoa huo.Alipohitimu masomo kule Makerere nchini Uganda alirudi kufundisha katika shule ya sekondari St. Marrys hapa Tabora. Vilevile kuna maamuzi muhimu ya kihistoria yaliyofanyika Tabora.

“Mwaka 1958 maamuzi yaliyofanywa na mkutano mkuu wa TANU kushiriki uchaguzi, maamuzi ambayo yalisogeza nchi yetu karibu na uhuru wake,”amesema Dk.Samia na kuongeza hayo yanathibitisha namna ambavyo CCM ina historia kubwa na Tabora.

“Mnara wa kumbukumbu wa maamuzi hayo ya busara ya TANU upo mkoani hapo hadi sasa.Mnara huo unaonyesha ukumbusho wa safari kuelekea uhuru wa kisiasa,”amesema Dk.Samia.

Amefafanua kuwa leo nchi yetu inaendeleza mapambano ya uhuru wa kujitegemea kiuchumi. “Tayari uhuru wa siasa tulishaupata mwaka 1961, leo tunakwenda katika mapambano ya kujitegemea uhuru wa kiuchumi.”

Dk.Samia Suluhu Hassan amesema kwamba “Uhuru wa kujenga taifa lenye uchumi jumuishi linalotegemea na linalozingatia ustawi wa watu wote. Na ndiyo maana tunasema Kazi na Utu, Tunasonga mbele.”

Amesisitiza CCM inataka kujenga taifa linalojitegemea na linalozingatia ustawi wa watu na katika mapambano hayo, amesema kuwa CCM inaendeleza yale ambayo Baba wa Taifa aliyasisitiza kwa kusema wananchi ni sisi sote kwa pamoja.

“Maendeleo ni yetu na juu yetu wenyewe. Maendeleo tunayoyataka ni maendeleo ya watu, yaletwe na watu wenyewe, yaendelezwe na watu wenyewe na yawafuate watu kule walipo,” amesema Dk.Samia na kuongeza hiyo ndiyo maana halisi ya uchumi jumuishi ambao CCM imedhamiria kuujenga kuleta maendeleo mijini na vijijini.

Ameongeza maendeleo hayo yaletwe na watu wenyewe ambao ni wananchi.Pamoja na hayo Dk.Samia ameendelea kuomba kura katika uchaguzi Mkuu kwa kumchagua Rais wa Jamhur i ya Muungano wa Tanzania,Wabunge na madiwani.

Pia ametoa rai kwa wingi huo huo unaoonekana katika mikutano na siku ya kupiga kura wajitokeze kwa wingi huo huo ili CCM ishinde ili iendelee kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.