Samia Aahidi Kuendeleza Maendeleo Tabora kwa Miaka Mitano Ijayo – Video – Global Publishers

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Manispaa ya Tabora imenufaika kwa kiwango kikubwa na miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita, huku akiahidi kuendeleza kasi hiyo katika miaka mitano ijayo endapo atachaguliwa tena Oktoba 29, 2025.

Akihutubia maelfu ya wananchi leo Ijumaa, Septemba 12, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Viwanja vya Ipuli mjini Tabora, Dkt. Samia amesema kukamilika kwa Hospitali ya Manispaa ya Tabora pamoja na majengo ya huduma za afya kumeimarisha upatikanaji wa matibabu. Ameongeza kuwa sekta ya elimu nayo imepiga hatua kubwa, ambapo shule za msingi zimeongezeka kutoka 819 mwaka 2020 hadi 960 mwaka 2025, na sekondari kutoka 197 hadi 277.

Amesema pia huduma za maji safi zimeimarika, upatikanaji wa mbolea na dawa za ruzuku kwa wakulima umeongezeka, huku mifugo ikinufaika na chanjo na maboresho ya huduma. Aidha, miradi ya ujenzi wa soko kuu na stendi, ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Tabora na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, vimekuwa nguzo muhimu za kuifanya Tabora kitovu cha maendeleo.

Akizungumzia mpango wa miaka mitano ijayo, Dkt. Samia ameahidi kujenga shule mpya nne, mabweni 16, nyumba 46 za walimu, vyumba 19 vya TEHAMA, maktaba 17 na majengo ya utawala 12 katika sekondari za Manispaa ya Tabora. Pia amebainisha kuwa serikali itakamilisha mradi wa mtandao wa maji safi na maji taka, kujenga barabara ya Tabora–Ipole–Koga–Mpanda (km 202), minada mitatu ya mifugo, majosho matano, malambo 20, mabwawa ya samaki 20 na soko la samaki moja.

“Dhamira yangu ni kuona kila sekta inagusa maisha ya wananchi wa Tabora. Tunataka maendeleo ya hospitali, shule, maji, kilimo, viwanda, mifugo na uvuvi yaende kwa kasi zaidi,” amesema Dkt. Samia.