Dar es Salaam. Wabunifu nchini wamehimizwa kuja na teknolojia zitakazochochea matumizi bora na sahihi ya nishati, ili kusaidia kupunguza upotevu na kuongeza ufanisi wa matumizi yake.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 12, 2025, katika hafla ya kuwapongeza washindi 10 wa shindano la ‘Energy Efficiency Innovation Challenge,’ linalolenga kuwahamasisha vijana wabunifu kuibua suluhisho za kiteknolojia kwa matumizi bora ya nishati.
Mashindano hayo, yanayofanyika kwa mara ya pili nchini, yanasimamiwa na Wizara ya Nishati kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Kila mshindi amezawadiwa Sh25 milioni kwa ajili ya kuendeleza teknolojia aliyoiibuni.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga amesema kuendelea kwa ubunifu wa teknolojia hizo kutasaidia kupunguza upotevu wa nishati na kuchochea matumizi yenye tija kwa jamii.

Ameongeza kuwa, kupitia ubunifu huo, vijana wanaweza kujiajiri, kuajiriwa, na hata kuwaajiri wengine, hivyo kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
“Bunifu hizo ni sehemu ya mkakati wa kuhamasisha matumizi bora ya nishati ambayo yatasaidia kuendelea kupunguza upotevu wa nishati,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali katika kuhakikisha bunifu hizo zinakuwa endelevu na zenye tija wamekuwa wakiwafuatilia kwa ukaribu na kuwasaidia wabunifu hao, ili teknolojia zao ziweze kunufaisha jamii.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo tutaendelea kuwatambua na kuhakikisha vijana hawa wanasaidiwa kukuza na kuboresha teknolojia zao ili ziweze kuwa na tija kwa jamii,” amesema.
Amesema upotevu wa nishati nchini umepungua hadi kufikia asilimia 14.8 kutoka asilimia 21 mwaka 2021.
Luoga amesema hayo ni matokeo ya ukuaji wa teknolojia na kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu matumizi bora na sahihi ya nishati.
“Siku hizi watu wameelimika wanatumia vifaa vinavyotumia umeme kidogo na teknolojia ya kisasa mfano taa ambazo mtu anapofunga mlango zinazimika na anapofungua zinawaka, hii inasaidia kupunguza matumizi yasiyo na lazima,” amesema.
Kwa upande wake Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP, John Rutere amesema wakati nchi ikiendelea kukua kwa kasi haswa katika upande wa viwanda, ni muhimu kuja na teknolojia zitakazoleta suluhu ya matumizi bora ya nishati.
“Hii ndiyo sababu iliyotusukuma kuwapa nafasi vijana wa Tanzania kuja na bunifu zitakazosaidia kuhamasisha matumizi ya nishati safi,” amesema.
Amesema watahakikisha teknolojia hizo zinazobuniwa na vijana zinatumika kimataifa kusaidia matumizi bora ya nishati.
Mkuu wa Rasilimali Asili wa Umoja wa Ulaya, Lamine Diallo amesema wao kama wadau wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha matumizi bora ya nishati yanafikiwa kwa kiwango kikubwa.
Mmoja wa washindi wa shindano hilo ambaye pia ni mhadhiri wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Dk Gadiana Phillipo amesema kumekuwa kukifanyika jitihada nyingi za kuhakikisha uzalishaji unaongezeka,kutumia teknolojia za kisasa utasaidia umeme uliopo kutumika vizuri.