Dodoma. Wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wakipaza sauti zao kutaka sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ifanyiwe marekebisho ili kumpa nafasi mtoto wa kike kupata elimu, Serikali imesema kuwa inafanya jitihada mbalimbali za kukamilisha mchakato huo.
Sheria hiyo ya ndoa imeruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 kuolewa kwa idhini ya Mahakama na mwenye umri wa miaka 15 kuolewa kwa idhini ya wazazi, huku ikipingana na sheria ya mtoto inayomtambua kuwa ni mwenye umri chini ya miaka 18.
Akizungumza kwenye kikao kazi cha wahariri wa vyombo vya habari na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali leo Ijumaa Septemba 12, 2025 Jijini Dodoma, rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA), Bavoo Junus amesema zipo jitihada zinazofanywa na Serikali.
Amezitaja jitihada hizo kwenye marekebisho ya sheria hiyo, ikiwemo kukusanya maoni kutoka kwenye makundi mbalimbali ya jamii.

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari wakiwa katika kikao kazi cha Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Serikali jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Amesema yapo mambo mengi yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya kurekebisha sheria hiyo ikiwemo imani na desturi za watu, hivyo kila kundi ni lazima lishiriki kabla ya marekebisho ili wakubalianae kabla ya kufanyika.
“Kwa kesi kama hii mimi ninachofahamu kwa sasa utaratibu unaoendelea chini ya Wizara ya Katiba na Sheria walikuwa wameandaa programu ya kukusanya maoni, kwa hiyo kuna hatua mbalimbali ambazo zimeshachukuliwa,” amesema.
Junus amesema kwa ujumla waandishi wa sheria wanafanya kila jitihada za kuona zinazotungwa zinakidhi mahitaji, kwa kushirikisha makundi yote yanayohusika.
Amewaasa mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwani wao ni kiungo kati ya jamii na Serikali, hivyo wanatakiwa kuwa waadilifu.
Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa uratibu na huduma za ushauri wa kisheria, Ipyana Mlilo amewataka mawakili wa Serikali kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili kwani wao ni daraja kati ya jamii na Serikali.

Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka akifuatilia jambo katika kikaokazi cha Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Serikali kwa wahariri wa vyombo vya habari jijini Dodoma.
Naye mhariri wa Clouds Media, Joyce Shebe amesema kikao kazi hicho kimewawezesha kukutana na Chama Cha Mawakili wa Serikali na kujifunza mambo mengi yanayohusiana na masuala ya kisheria ikiwemo utatuzi wa migogoro mbalimbali inayoikabili jamii.
“Kwenye shughuli zetu za kila siku huwa tunakutana na watu wanaohitaji msaada wa kisheria na sisi siyo wanasheria, hivyo tutawaelekeza kwenu ili wapate msaada. Lakini msaada wa kisheria unahitajika sana kwa jamii kwa sababu wapo watu wengi ambao wana changamoto za kisheria lakini hawajui pa kuanzia,” amesema Shebe.