JKCI yarejesha tumaini la watoto 28 kwa kuwafanyia upasuaji wa moyo

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa zaidi ya Sh250 milioni baada ya watoto 28 wenye matatizo ya moyo, ikiwemo matundu, mishipa na vyumba vya moyo, kufanyiwa upasuaji nchini na madaktari bingwa kutoka King Salman Foundation ya Saudi Arabia.

Mbali na upasuaji, taasisi hiyo imenufaika na msaada wa vifaatiba vyenye thamani ya takriban Sh70 milioni, ambavyo vitaongeza uwezo katika utoaji wa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo.

Akizungumza leo Septemba 12, 2025, katika hafla ya kuwaaga madaktari hao, Mwahija Abdallah  mkazi wa Tanga, aliyenufaika na huduma hiyo kwa niaba ya wazazi wengine  amesema msaada huo umepunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa gharama za matibabu.

Ameeleza kuwa mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili alihitaji Sh9 milioni kwa ajili ya upasuaji wa moyo, lakini kupitia msaada huo amelipa Sh1 milioni pekee.

“Wametuletea furaha kubwa, watoto wetu wamerudi na matumaini mapya. Furaha ya watoto wetu ndiyo furaha yetu, hatuna cha kuwalipa, ila Mwenyezi Mungu awalipe mema kuliko yote,” amesema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema upasuaji uliofanyika ni faraja kubwa kwa familia na Taifa kwa ujumla.

“JKCI sasa imeendelea kuwa taasisi bora si tu nchini Tanzania bali Afrika Mashariki na Kati, ikiwa ya kwanza kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto na watu wazima,” amesema Dk Kisenge.

Naye, Naibu Balozi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Abdallah Gashan amesema mafanikio hayo ni ya kujivunia kwa kuwa yameokoa maisha ya watoto na kurejesha tabasamu kwa familia nyingi nchini.

“Tunatoa shukurani kwa Serikali ya Ufalme wa Saudi Arabia na washirika wote waliowezesha mafanikio haya. Vilevile, tunawapongeza madaktari na wahudumu wote waliotoa muda na utaalamu wao kuokoa maisha ya watoto hii ni fahari kubwa kwa mataifa yetu,” amesema Gashan.

Aidha, amesisitiza kuwa Saudi Arabia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya afya ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na huduma za kibingwa.