Tanga. Watalaam wa kilimo na ushirika kutoka halmashauri 11 za Mkoa wa Tanga wamebainisha mazao yatakayowasaidia wananchi hususan wakulima kuinua uchumi wao.
Akizungumza kwenye kikao kilichojumuisha wataalamu wa kilimo, ushirika na wadau wengine kilichofanyika leo Septemba 12, 2025 wilayani Handeni mkoani Tanga, Ofisa kilimo Mkoa, George Mmbaga amesema lazima wakulima wasaidiwe ili kulima kilimo chenye tija.
Amesema wamekaa na kujadiliana na kuona yapo mazao ambayo mkulima akijikita nayo, yatamuinua kiuchumi kwani soko lake lipo.

Baadhi ya maofisa kilimo na ushirika kutoka halmashauri 11 za mkoa wa Tanga wakiwa kwenye kikao cha kujadili mipango ya kukuza sekta ya kilimo kwa mwaka 2026 ikiwemo kuongeza thamani ya mazao. Picha na Rajabu Athumani
Ametaja mazao ya kipaumbele ya Mkoa wa Tanga kuwa ni korosho, mpunga, mahindi, mihogo, mkonge, ufuta, mbogamboga na matunda kwani yanakubali kwenye maeneo mengi ya mkoa huo.
“Mazao haya yameelezwa kuwa na nafasi kubwa katika kuchochea uchumi wa wakulima na kuongeza pato la Mkoa wa Tanga kila mkulima, akijikita kufanya kilimo hiki, ataweza kupata faida kubwa na sisi kama wataalamu twende tukasimamie haya,” amesema Mmbaga.
Amesema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2025 Mkoa wa Tanga uzalishaji wa mpunga ni asilimia 37 na korosho kwa asilimia 44, huku ushirika ukiimarika kwa zaidi ya vyama 135 vya msingi vilivyosajiliwa na kuanza kutoa huduma bora kwa wanachama wake.

Baadhi ya maofisa kilimo na ushirika kutoka halmashauri 11 za mkoa wa Tanga wakiwa kwenye kikao cha kujadili mipango ya kukuza sekta ya kilimo kwa mwaka 2026 ikiwemo kuongeza thamani ya mazao. Picha na Rajabu Athumani
Katibu tawala msaidizi, uzalishaji Mkoa wa Tanga, Emigiudius Kasunzu amesema sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa wananchi wa Tanga, hivyo jitihada zote lazima zielekezwe katika kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao.
Amesema lazima wawekeze katika kilimo chenye tija kupitia mazao hayo ya kipaumbele, na wanatarajia kuongeza zaidi ya asilimia 20 ya uzalishaji ifikapo mwaka 2026, sambamba na kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo.
Ofisa Ushirika wa halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Fraterne Minde amesema kwa mwaka 2026 watazidi kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani, hasa kwenye zao la mkonge kwa kutafuta na kuunganisha vyama na bodi ya mkonge ili waweze kupata wanunuzi wa zao hilo kwa bei rafiki kwa wakulima.
Ofisa Ushirika Tanga Jiji, Evarist Mushi amesema zao ambalo pia watakwenda kutoa kipaumbele kwa mwaka ujao na kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani ni korosho lengo ni kuwanufaisha wakulima wengi.
Amesema watatoa elimu ya fedha kwa wanachama wa vyama vya ushirika ili waweze kujiepusha na mikopo inayowaumiza maarufu kama ‘kausha damu’ ili kuweza kupata faida zaidi.
Kwenye kikao hicho wataalamu hao wameazimia mwaka 2026 utakuwa wa kuongeza thamani ya mazao kupitia viwanda vidogo vya kusindika, kuimarisha huduma za ugani na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa wakulima.