Mahakama yabariki faini 30,000 bajaji iliyoegeshwa isivyostahili

Moshi. Ni kama utamaduni wa baadhi ya madereva wa pikipiki za magurudumu matatu maarufu bajaji kuegesha vyombo vyao vya moto popote, lakini bahati haikuwa ya Boniface Mtafya, kwani kosa hilo limemfikisha mahakamani alikotozwa faini ya Sh30, 000.

Moshi ni miongoni mwa miji nchini Tanzania, ambayo inakabiliwa na msongamano wa bajaji kutokana na wingi wake kuliko uwezo wa barabara zake, huku madereva walio wengi wakikiuka sheria za usalama barabarani.

Madereva hao husimama popote, tena ghafla, kupakia abiria na wakati mwingine wakisimama katikati ya barabara hasa za YMCA-KCMC, Nyerere na eneo la Bora. Hali hiyo husababisha msongamano wa magari na bajaji.

Hali kama hiyo inaikumba miji mingine kama vile Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza, Iringa, Kigoma, Geita na mikoa mingine, ambako bajaji hutumika kama daladala na kusimama popote kupakia abiria, bila kujali watumaiji wengine wa barabara.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki na Waendesha Bajaji na Bodaboda Kilimanjaro (CWDK), Bahati Nyakiraria amepongeza hukumu iliyotolewa na mahakama, akisema adhabu za aina hiyo zinatoa fundisho kwa wengine.

“Tuna changamoto kubwa hasa baada ya faini kushuka kutoka Sh30,000 hadi Sh10,000, wapo madereva bajaji na bodaboda wanarudia makosa yaleyale waliyotozwa faini. Hili kosa la kuegesha popote kupakia abiria limekuwa sugu,” amesema na kuongeza:

“Bahati nzuri hii kesi iliamuliwa na Mahakama ya Wilaya ya Moshi, mtu hakuridhika amekata rufaa Mahakama Kuu na imebariki adhabu. Nadhani kuna haja ya kuwa na data bank (kanzi data) ya wanaopatikana na hatia hata kama walilipa faini polisi.”

Uendeshaji wa baadhi ya madereva bajaji na bodaboda umekuwa ukilalamikiwa karibu nchi nzima kwa kufanya makosa ya wazi ya usalama barabarani yanayochangia ajali, ambazo kati ya Januari hadi Desemba 2024 zilitokea 383 Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa takwimu za kati ya Januari na Desemba 2024 zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ajali za pikipiki zilisababisha vifo vya watu 352, huku matukio ya uendeshaji wa vyombo hivyo kwa uzembe yalikuwa 765.

Novemba 7, 2023, Mtafya akiendesha bajaji aina ya TVS uelekeo wa KCMC, alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa mawili ya barabarani na kupatikana na hatia katika kosa la pili aliloshitakiwa nalo.

Kosa la kwanza lilikuwa kubeba abiria zaidi ya idadi iliyoidhinishwa na kanuni ya 15(c) ya sheria ya Kanuni za Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra) za mwaka 2020 zinazohusu kutoa huduma ya ukodishaji wa usafiri kama ilivyo usafiri wa teksi.

Kuhusu kosa la pili, siku hiyohiyo, Mtafya alishtakiwa kwa kosa la kuegesha bajaji eneo lisiloruhusiwa. Alidaiwa aliegesha pikipiki kwa uzembe na bila kuzingatia watumiaji wengine wa barabara hiyo.

Ushahidi unaonyesha siku hiyo, kiongozi wa waendesha bajaji njia ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Aidano Mdoe, akiwa hapo, aliona bajaji iliyokuwa ikiendeshwa na Mtafya ikisimama na kupakia abiria watano, badala ya watatu.

Alimsimamisha dereva huyo na kumhoji lakini hakuwa na majibu ndipo alipowasiliana na ofisa wa Trafiki, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Mahenda Kera ambaye alifungua jalada, lakini pia alihusishwa Ofisa Mkuu wa Latra, Paulo Nyello.

Nyello alipokagua leseni ya usafirishaji kutoka Latra alibaini ni ya kufanya biashara eneo la Rau na si Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kama alivyokutwa siku hiyo.

Katika utetezi wake, alieleza siku ya tukio akiwa amebeba abiria watatu akitokea mjini kuelekea Chuo Kikuu cha Ushirika, alikutana na watu watano ambao walimuamuru ashushe abiria, wakisema bosi wao amewaagiza hivyo.

Baada ya usikilizwaji kamili wa kesi hiyo, alipatikana na hatia katika shtaka la pili na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh30,000 au kifungo cha miezi sita jela.

Mshtakiwa hakuridhika na adhabu hiyo akaamua kukata rufaa Mahakama Kuu.

Katika sababu zake za rufaa, alieleza hakimu alikosea kisheria kumtia hatiani kwa kuegemea ushahidi ambao haukuthibitisha shtaka na pia alikosea kwa kumtia hatiani pasipo kuzingatia kikamilifu ushahidi wa mrufani wakati alipojitetea.

Katika hukumu ya rufaa iliyotolewa Septemba 9, 2025 na hukumu hiyo kuwekwa katika mtandao wa mahakama leo Septemba 12, Jaji Adrian Kilimi alitupilia mbali rufaa akisema Jamhuri ilithibitisha shtaka hilo.

Jaji Kilimi amesema baada ya kupitia na kuchambua ushahidi uliomtia hatiani mrufani, haibishaniwi kuwa mrufani alikutwa eneo la Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi akifanya biashara ya kubeba abiria kwa kutumia bajaji.

Jaji amesema pia ni suala lisilo na ubishani kuwa stika ya leseni yake ilionyesha anapaswa kubeba abiria eneo la Rau-Vet, hivyo swali linabaki kuwa ni je, alipatikana na hatia ya kuegesha bajaji eneo lisiloruhusiwa?

Akirejea ushahidi, Jaji Kilimi amesema kulingana na ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, hususan shahidi wa kwanza, Aidano Mdowe, mrufani aliegesha bajaji eneo la Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi wakati siyo njia yake.

Ukiacha ushahidi huo, maelezo yake ya onyo aliyoyaandika Polisi ambayo yalipokewa mahakamani kama kielelezo, yanajieleza alikiri leseni yake ni ya kusubiria abiria Rau Madukani na si eneo ambalo alikutwa.

Katika maelezo hayo aliulizwa nani alimpa mamlaka ya kwenda kuegesha bajaji eneo la ushirika, naye akajibu alipewa na watu wa Halmashauri ya Manispaa Moshi, ingawa hawakumpa kibali cha maandishi bali kwa mdomo.

Swali lingine katika maelezo hayo aliulizwa kama anatambua amekiuka masharti ya leseni ya usafirishaji na ni kosa kwa mujibu wa sheria, naye akajibu: “Ndiyo natambua ni kosa kwa mujibu wa sheria.”

Jaji Kilimi amesema kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na maelezo ya mrufani, anaridhika kuwa kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa pasipo kuacha shaka kwa sababu hakuwa na leseni ya kuegesha eneo alilokutwa.

Jaji amesema haoni sababu ya kubatilisha kile ambacho mahakama ya awali ilikifikia na kwamba, rufaa yake haina mashiko na inatupiliwa mbali.

Mahakama imebariki kutiwa kwake hatiani na adhabu aliyopewa.