Pacome wa mwisho akifungwa kamba na Manara

NI zamu ya Pacome Zouzoua kufungwa kamba ya viatu na Haji Manara katika utambulisho wa wachezaji msimu huu wa 2025/26 unaotarajia kuanza Septemba 17 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Msimu uliopita Manara alifanya hivyo kwa Stephane Aziz Ki, na pia aliwahi kufanya hivyo kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ wakati huo akiwa Yanga na Clatous Chama enzi zile akiwa Simba, ambapo leo katika kilele cha Mwananchi amefanya hivyo kwa Pacome.

Msemaji huyo wa zamani wa Yanga an Simba amefanya hivyo wakati akitambulisha kikosi cha wachezaji 30 wa Yanga ambapo wakati wa kumfunga kamba Pacome mashabiki waliibua shangwe kwa kumuita “MVP MVP”.

“Nimewaona wachezaji wengi akiwemo Sunday Manara, Pacome ni mchezaji mzuri sana,” hiyo ilikuwa ni sehemu ya maneno ya Manara baada ya kukamilisha utambulisho wa wachezaji ambapo Pacome hakumuita jukwaani kama wengine, bali alimfuata katika vyumba vya wachezaji na kupanda naye eneo lililokuwa na wachezaji wote.

TSHABALALA AIBUA SHANGWE
Wakati nyota wote wakiteka hisia kwa kushangiliwa na mashabiki, aliyekuwa nahodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliibua shangwe akipokewa kwa shangwe na sehemu ya sauti ya muziki ambao ulimfanya acheze.

Tshabalala alipoitwa na Manara kutoka ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo, mashabiki walimpokea kwa kelele wakimkaribisha Jangwani na yeye aliwajibu kwa kuwapa burudani akicheza muziki uliokuwa ukipigwa.

Katika kundi la nyota 30 waliotambulishwa limeibuka jina la Yao Kouasi ambaye inaelezwa kuwa ameondolewa kwenye mfumo kupisha usajili wa nyota wengine 12 wa kigeni watakaocheza msimu huu.

Wachezaji wa Yanga kwa msimu huu ni  Bakari Mwamnyeto, Djigui Diarra, Mshery, Abubakar Khomen, Israel Mwenda, Kibwana Shomari, Shadrack Boka, Abdallah Hamad Bacca, Ninju, Dickson Job.

Wengine ni Frank Asink, Aziz Andambwile, Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’, Abubakar Salum ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya, Denis Nkane, Farid Mussa, Shekhan Khamis, Effen Chikola, Balla Conte, Duke Abuya, Edmund George, Celestin Ecua, 
Mohammed Doumbia, Prince Dube, Andy Boyeli, Maxi Nzengeli na Clement Mzize.