Majaliwa: Tutasaka kura Kitanda kwa kitanda

Nachingwea. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kitasaka kura kwa namna yoyote ile hata kama ni nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda shuka kwa shuka katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizindua kampeni katika Wilaya ya Nachingwea leo Ijumaa Septemba 12,2025 Majaliwa amesema kuwa wanaCCM wanatakiwa kusaka kura za Rais, wabunge na madiwani ili viongozi hao wakawaletee wananchi maendeleo.

Ameendelea kusema kuwa wamchague Fadhili Liwaka mgombea ubunge wa Nachingwea ili kuendeleza pale alipoachia mtangulizi wake.

“Liwaka namjua vizuri sana mchapakazi mno mchagueni  ili aweze kuendeleza pale alipoachia mtangulizi wake ili kuendeleza miradi iliyobakia na kuondoa changamoto za Jimbo la Nachingwea.”

Pia Majaliwa amewataka WanaCCM kutobweteka kwa maeneo ambayo wamepita bila kupingwa, waendelee kufanya kampeni hadi siku ya uchaguzi, kwani kupita bila kupingwa sio sababu ya kutofanya kampeni.
Kwa upande wake mbunge aliyemaliza muda wake, Amandus Chinguile ameahidi kumnadi     Liwaka ili apate ushindi wa kishindo.

“Nitahakikisha nampigia kampeni Liwaka hadi kieleweke  na watashinda kwa kishindo kuanzia kura za Rais, madiwani na mbunge.”amesema Chinguile.


Kwa upande wake Liwaka amesema akipata ridhaa ya kuingia bungeni kipaumbele chake cha kwanza ni kujenga barabara ya Nachingwea -Masasi kwa kiwango cha Lami, ujenzi wa mabweni ya watoto wa kike kwa kila sekondari pamoja kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji.