Mirerani. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Almas Kisabya amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais, ataunda Serikali ndogo yenye wizara zisizozidi 10, lengo likiwa kufanikisha utendaji kazi.
Kisabya ameyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni ya urais leo Ijumaa Septemba 12 mwaka 2025 mjini Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, ataunda Serikali yenye wizara chache ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama zisizo na ulazima.
Amezitaja wizara hizo ni Wizara ya Jamii, Wizara ya Mambo ya Hovyo, wizi, uzembe na uvivu, Wizara ya Elimu na Sayansi, Wizara ya Fedha na Wizara ya Ujenzi.
Amezitaja nyingine ni Wizara ya Afya na mazingira, Wizara ya Muungano, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Mambo ya Nje na Utalii na Wizara ya Katiba na Sheria.
“Pamoja na wizara chache nitaunda Serikali isiyo na ubaguzi kwani itakuwa na mawaziri wa vyama vyote ya umoja wa kitaifa kwani Taifa kwanza vyama baadaye,” amesema Kisabya.
Amesema anataka maisha ya Watanzania yasiendeshwe na wanasiasa na nchi isiwe sehemu ya kupeana zawadi, hivyo atakuwa na mawaziri wachache na wataalamu wengi.
Pia, amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, Serikali yake haitadai fedha kwa ajili ya maiti au wafu hospitali bali kusitiriwa kwa heshima.
“Sasa hivi mtu akifiwa anakuwa analia mara mbili kwani anakuwa amempoteza ndugu yake na pia analia juu ya namna ya kulipia gharama za matibabu kabla ya msiba,” amesema.
Amesema Serikali yake itatoa kipaumbele kwa watu watakaofiwa kwani maiti zitatolewa kwenda kuzikwa bila kudaiwa fedha zozote.
“Kila mmoja ni maiti mtarajiwa na tafsiri ya kimungu maiti ni mtu aliyestaafu duniani, anapaswa kusitiriwa kwa kuondoka kwa heshima na siyo kung’ang’aniwa kwa sababu ya madeni,” amesema Kisabya.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro kwa tiketi ya NRA, Zaituni Fundikira amesema endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo atawatetea wachimbaji madini ya Tanzanite.
Fundikira amesema rasilimali ya madini ya Tanzanite ipo mji mdogo wa Mirerani, hivyo inapaswa kuwanufaisha Watanzania kwa ujumla na jamii ya eneo hilo.
Mmoja kati ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, Juma Ally ambaye ameshiriki mkutano huo amewapongeza viongozi hao kwa kutoa sera zao na si kushambulia watu binafsi au vyama vya kisiasa.
“Mkutano ulikuwa mzuri kwani wagombea wameeleza nini watawafanyia Watanzania endapo watachaguliwa kushika nafasi zao na siyo kutoa kashfa wala matusi,” amesema.