Takriban saa nzima ya Zuhura Othuman maarufu Zuchu katika tamasha la Wiki ya Mwananchi imetosha kutoa burudani ya aina yake kabla ya mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Yanga na Bandari FC.
Zuchu ametumia majukwaa manne tofauti akiimba nyimbo zake zaidi ya sita, huku akimrudisha jukwaani kwa mara ya pili D Voice kuimba naye wimbo walioimba pamoja.
Mwanadada huyo ameonyesha ubora wa kuimba laivu pamoja na kutumia vyombo, huku akitoa burudani kwa mashabiki kibao waliojitokeza katika Uwanja wa Mkapa.
Msanii huyo kutoka WCB hajaingia kinyonge uwanjani kwani ameingia akiwa amefungiwa kwenye kiota ambacho kilifunguliwa muda mfupi baada ya kufika eneo husika la majukwaa ambayo yaliyaandaliwa kutumika kwa ajili ya kutumbuiza.
Ukiondoa uburudishaji wake mwanadada huyo akihama kwenye majukwaa manne alifanya hivyo pia kwenye mavazi akibadilisha mara nne.
Staa huyo ambaye alikuwa na madansa wengi wa kike na wa kiume hakuishia tu katika kuimba, pia alionyesha uhodari wake wa kucheza na kuyamudu majukwaa hayo, jambo ambalo limemuonyesha kuwa na pumzi ya kutosha.
Zuchu aliomba kuzimiwa taa za uwanja kwa muda akiomba utulivu kutokana na kuandaa jukwaa la kuimba lavu jambo ambalo liliibua hisia za shangwe kwa mashabiki.