Fadlu ana saa 72 za uamuzi

KABLA ya mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga, kocha wa Simba, Fadlu Davids na benchi la ufundi la timu hiyo wana siku tatu ngumu ambazo ni sawa na saa 72 ili kuandaa furaha kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi.

Simba iliyopoteza katika mechi tano mfululizo dhidi ya Yanga katika mashindano yote itakutana tena na watani wake hao Jumanne ya wiki ijayo, Septemba 16 kufungua pazia la msimu mpya.

Licha ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya mwisho ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya kuna upungufu kadhaa ulioonekana kiuchezaji kitimu mbali na ubora ulionekana wa mchezaji mmoja mmoja kama vile Naby Camara, Rushine De Reuck, Anthony Mligo na Yakoub Suleiman waliong’ara.

Kilichoonekana ni kwamba Simba haikuwa vizuri kimuundo hasa katika kipindi cha pili. Kikosi kilionekana kugawanyika vipande pale waliposhindwa kumiliki mpira kwa muda mrefu, jambo linalodhihirisha kuwa bado hawajapata muunganiko wa kiuchezaji. Changamoto hiyo inaonekana kuchangiwa na maingizo mapya yaliyosajiliwa msimu huu. Wachezaji kama Neo Maema na wengine hawajaingia vizuri kwenye mfumo wa kikosi.

Jambo lingine lililojitokeza ni namna Fadlu anavyopambana kutengeneza mfumo wake mpya wa kuanza na washambuliaji wawili wa kati. Katika mechi dhidi ya Gor Mahia aliwajaribu washambuliaji wote wa mwisho, alianza na Sowah na Kibu wote wakicheza mbele.

Baadaye waliingia na kucheza kwa vipindi tofauti, Seleman Mwalimu na Steven Mukwala. Kwenye karatasi, mfumo huu unatoa matumaini ya kuongeza nguvu ya kushambulia, lakini kwenye uhalisia bado unaonekana na changamoto kwenye utekelezaji.

Sababu kubwa ni washambuliaji hao bado hawajapata muunganiko  wa kutosha. Wakati mwingine walionekana kuingiliana maeneo na mara nyingine wakabaki wakiwa mbali mno na eneo la mwisho mfano Sowah katika dakika 45 za kipindi cha kwanza alionekana kushuka chini zaidi kutafuta mipira baada ya Charles Jean Ahoua na Maema kushindwa kumtengenezea nafasi za mabao.

Fadlu anatakiwa kuhakikisha kuna uwiano kati ya nguvu ya washambuliaji wawili na nidhamu ya wachezaji wa kati wanaotakiwa kuwasaidia.

Aidha, mfumo wa 4-4-2, anaoupa kipaumbele unahitaji viungo wabunifu wenye pumzi ya kutosha, wanaoweza kushambulia na kulinda kwa ufanisi. Ndiyo maana changamoto ya pili kwa Simba ni namna ya kupata viungo watatu wa kati watakaoshirikiana bila kupoteza mpangilio.

Ndani ya siku tatu zijazo, lazima Fadlu ajue nani anafaa kubeba jukumu hili.

Ukiangalia rekodi za hivi karibuni, Simba imekuwa ikipoteza udhibiti wa kiufundi kila inapokutana na Yanga. Mara nyingi Yanga imefaidika na safu ya viungo yenye uwiano bora, hali iliyoifanya iwe na uhuru wa kumiliki mpira na kuamua kasi ya mechi.

Ikiwa tatizo hili halitatatuliwa, Simba inaweza kujikuta ikirudia makosa yale yale kwenye Ngao ya Jamii.

Lakini zaidi ya kubadili mfumo, Simba inahitaji utulivu kwa wachezaji wao. Timu hii mara nyingi imekuwa ikianza mechi kubwa vizuri, lakini inapopoteza umakini kwa dakika chache, mfano mzuri ni msimu uliopita katika mechi kama hii ya Ngao ya Jamii.

Kwa siku tatu zilizobaki, Simba italazimika kufanya kazi kwenye uwiano wa viungo wa kati na nidhamu ya washambuliaji. Bila hivyo, mfumo wa washambuliaji wawili unaweza kubaki kuwa mzuri kwenye karatasi lakini dhaifu kwenye uhalisia.

Kwa jumla, Fadlu Davids anakabiliwa na mtiani wa kuunganisha wachezaji wapya, kuhakikisha mfumo wa washambuliaji wawili unakuwa na uwiano sahihi, na kuondoa rekodi mbaya ya kupoteza mara tano mfululizo dhidi ya Yanga. Ni mitihani mizito, lakini ndiyo mizani itakayopima uimara wake kama kocha mkuu wa Simba.

Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo, Fadlu alisema; “Ni mechi muhimu ambayo itatupa mwelekeo mzuri wa kikosi chetu, kuna mambo ambayo tumeyaona katika  mechi iliyopita tutayafanyia kazi naamini huu ni  msimu mzuri kwetu na wenye mafanikio.

Kuhusu Ishu ya kucheza na washambuliaji wawili wa kati kocha huyo alisema huo ni uamuzi ambao umetokana na ubora wa washambuliaji wa mwisho walionao.

Kwa ujumla Simba ina wachezaji wanne wenye uwezo wa kusimama kama washambuliaji wa mwisho ambao ni Sowah, Mukwala, Mwalimu na Kibu.