KOCHA wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema mshambuliaji wa timu hiyo, Valentino Mashaka ni mmoja wa wachezaji ambao taifa litajivunia hivi karibuni kutokana na kipaji chake, huku akimtabiria kufanya makubwa msimu huu kama atatuliza akili na kupiga soka.
Ally alisema katika kikosi hicho ana nafasi ya kucheza na kuonyesha kiwango chake, lakini anachotakiwa Mashaka ni kuituliza akili yake kazini na kujua yupo timu nyingine.
Mashaka amejiunga na JKT Tanzania kwa mkopo akitokea Simba ambako msimu uliopita alifunga mabao mawili na hakuwa na nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza chini ya kocha Fadlu Davids.
“Tofauti na Simba ambako hakuwa na nafasi kubwa ya kucheza huku JKT Tz ni yeye kubadilisha akili yake kwa uharaka, ajitume kwa bidii na kujua kazi ya soka haina makao maalumu,” alisema Ally na kuongeza:
“Bado ni kijana umri wake unamruhusu kuzipambania ndoto zake, kila fursa anayopata ya kucheza akiitazama kwa jicho la kufika mbali atawashangaza Watanzania katika msimu unaotarajia kuanza Septemba 17.”
Mbali na Mashaka alimzungumzia na Saleh Karabaka aliyemaliza msimu uliyopita na mabao mawili aliyofunga Simba kabla ya kupelekwa kwa mkopo Namungo FC anaamini akijituma kwa bidii kipaji chake kitakwenda kuonekana kwa ukubwa.
“Kazi yangu ni kuona kila mchezaji aliyepo katika timu anafanikiwa kufanya vizuri kwa kuwajenga kiakili na kuwapa mbinu za uchezaji,” alisema Ally aliyeiwezesha JKT kumaliza nafasi ya sita katika Ligi Kuu 2024/25.