Fountain Princess yabeba kiungo Iringa

FOUNTAIN Gate Princess iko kambini Dodoma ikijiandaa na maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake, lakini kuna sura mpya zimeonekana kambini.

Timu hiyo msimu uliopita ilimaliza nafasi ya saba na katika mechi 18 ilishinda mechi sita sare mbili na kupoteza 10 ikikusanya pointi 20.

Miongoni mwa sura mpya ni pamoja na kiungo mshambuliaji Zainabu Dotto ambaye msimu uliopita aliitumikia Ceasiaa Queens alikokuwa kwa misimu miwili mfululizo.

Mwanaspoti ambalo lilifika kambini lilizungumza na kocha mkuu Noah Kanyanga aliyethibitisha kuwa kiungo huyo atakuwa naye msimu huu na tayari wamempa mkataba wa mwaka moja.

“Tumesajili wachezaji wengi wadogo lengo ni kurudisha Fountain kwenye makali yake. Zainabu tutakuwa naye kwa sababu ni mchezaji mzuri, wengine bado kuna vitu hatujakamilisha kwa sababu ni mchakato mrefu na unahitaji pesa,” alisema Kanyanga na kuongeza:

“Kama tutawapata wachezaji tunaowataka nafikiri tunaweza kuwa na msimu bora, wengi tuliowataka hadi sasa mambo yako vizuri tunashubiri msimu mpya tu.”

Msimu uliopita Dotto alicheza mechi 10 akifunga mabao matatu na asisti nne, chama lake likimaliza nafasi ya sita na pointi 21.