Ibrahim Ajibu aanza tambo mapema

KIUNGO mshambuliaji wa KMC, Ibrahim Ajibu ameweka wazi atakuwa na msimu bora katika kikosi hicho akipewa nguvu na ubora wa usajili uliofanywa na uongozi wa timu.

Ajibu msimu 2025/26 ataitumikia KMC baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja na amejiunga na timu hiyo akitokea Dodoma Jiji.

Pia amewahi kucheza klabu kadhaa hapa nchini zikiwemo Simba, Yanga, Azam, Coastal Union na Singida Big Stars.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ajibu alisema malengo aliyonayo msimu huu ni kuwa sehemu ya wachezaji watakaoipa mafanikio KMC na ameitaja timu hiyo itakuwa miongoni mwa zitakuwa tishio msimu ujao Ligi Kuu Bara.

“Ni nafasi nzuri kwangu kuonyeasha kile kilichoonwa na viongozi ambao wamenipa nafasi ya kucheza timu hii na nafurahi kuwa sehemu ya timu ambayo imefanya usajili mzuri, tusubiri mashindano yaanze lakini matumaini ya kufanya vyema ni makubwa sana,” alisema Ajibu.

Akizungumzia mikakati yake kama mchezaji, Ajibu alisema anaendelea na mazoezi  akishirikiana na wenzake ili ligi ikianza aweze kufanya kweli na kuisadia timu kumaliza katika nafasi za juu.

Nyota huyo aliyemewahi kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars kwa nyakati tofauti amelipongeza pia benchi la ufundi la timu yake linaloongozwa na kocha mkuu, Marcio Maximo.

“Benchi la ufundi linaongozwa na kocha mzoefu ambaye tayari analifahamu vyema soka la Tanzania matarajio ni makubwa na lengo ni kuhakikisha tutafika malengo ambayo tumejiwekea,” alisema Ajibu.