NUSU fainali ya michuano ya Kombe la Cecafa Kagame inachezwa leo baada ya kupigwa dochi kwa siku moja kupisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi, kwa kupigwa mechi mbili kwenye Uwanja wa KMC, huku macho yakitupiwa pambano la KMC na Singida Black Stars.
Mechi hiyo inawakutanisha makocha wenye heshima kubwa nchini, Marcio Maximo na Miguel Gamondi wanaozinoa timu hizo, huku pambano jingine likihusisha Al Hilal ya Sudan dhidi ya APR ya Rwanda litakalochezwa mapema mchana kwenye uwanja huo.
Mechi ya kwanza itakuwa ya kisasi kwa Al Hilal ambayo msimu uliopita ilifungwa na APR katika hatua kama hiyo na kushindwa kutinga fainali kabla ya Wanyarwanda hao kupoteza mbele ya walioibuka wababe wa Kagame Cup 2024, Red Arrows ya Zambia.
Al Hilal ilitinga nusu fainali kwa mara nyingine kutokana na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Kator ya Sudan Kusini.
APR iliyomaliza kinara wa Kundi B itakuwa na kibarua cha kutaka kuendeleza ubabe, huku ikiwa na hesabu za kusaka taji la nne la michuano inayohusisha klabu za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwani tayari imeshatwaa mara tatu 2004, 2007 na 2010.
Baada ya mechi hiyo ya mapema kivumbi kitakuwa katika nusu fainali ya pili ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano haya, makocha Marcio Maximo na Miguel Gamondi watakutana mmoja akiwa na KMC na mwingine Singida BS.
Singida BS, inayoshiriki kwa mara ya pili michuano hii, iliianza safari kwa suluhu dhidi ya Coffee ya Ethiopia kisha ikaipiga Polisi Kenya inayonolewa na kocha Etienne Ndayiragije mabao 2-1 kabla ya kumaliza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Garde Cotes ya Djibouti.
Kwa upande wa KMC, vijana hao wa Kinondoni walianza vyema wakiiangusha Mlandege ya Zanzibar kwa mabao 3-2, kisha wakaendeleza ubabe dhidi ya Bumamuru ya Burundi kwa ushindi wa bao 1-0 na kumaliza hatua ya makundi kwa sare ya 1-1 dhidi ya APR ya Rwanda.
Ingawa wote walikusanya pointi saba, lakini Singida Black Stars iliibuka kinara wa Kundi A wakati KMC ikishika nafasi ya pili Kundi B nyuma ya APR ikizidiwa mabao.
Kwa mujibu wa kanuni, timu tatu zilizomaliza kileleni mwa makundi ndizo hufuzu moja kwa moja, na moja bora zaidi kutoka nafasi ya pili huongezwa nafasi ambayo imechukuliwa na KMC.
Hii ni mechi inayosubiriwa kwa hamu na wengi kutokana na historia ya makocha hawa wawili. Gamondi, aliyeipa Yanga mataji matatu msimu wa 2023/2024 ambayo ni Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii, sasa anataka kufikisha Singida fainali ya kwanza ya Kagame.
Gamondi pia ndiye aliyeweka historia kwa kuifikisha Yanga, robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka mingi kifanya hivyo mara mbili mfululizo.
Akizungumza mechi hiyo Gamondi alisema; “Ninaiheshimu KMC, ni timu iliyopambana hadi kufika hapa. Kwetu hii itakuwa mechi nzuri pia ya kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa mashindano ya kimataifa, itakuwa jambo zuri kwetu kufika fainali ya mashindano haya pia hata kuchukua ubingwa.”
Kwa upande wa Maximo aliyewahi kuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu za vijana za Brazil miaka ya 1990 na kuja nchini 2006 kuinoa Taifa Stars hadi 2010 na kurejea kuinoa Yanga miaka 10 iliyopita, japo aliondolewa baada ya mechi ya Nani Mtani Jembe alipopoteza kwa Simba.
Mbrazili huyo alipata mafanikio enzi akiinoa Taifa Stars na kuipeleka fainali za CHAN 2009 kwa mara ya kwanza baada ya kuiondoa Sudan kwa jumla ya mabao 5-2, ambapo akizungumzia nusu fainali hiyo ya meo alisema: “Tunajua tunakutana na timu yenye kocha mwenye uzoefu mkubwa lakini KMC haipo hapa kwa bahati mbaya, tumepambana na tunataka kuandika historia yetu.”
Mechi hiyo pia itakuwa kipimo cha ubora wa wachezaji nyota wa timu zote mbili.
Kwa KMC, Kelvin Tondi Revocatus na Erick Mwijage ndio waliobeba matumaini yao huku Singida ikiwategemea mshambuliaji mpya, Horso Mwaku Malanga na kiungo, Clatous Chama.