KIPA wa zamani wa Yanga Princess, Adrophina Samson amejiunga na Ruangwa Queens kwa mkataba wa miaka miwili.
Timu hiyo imepanda Ligi Kuu ya Wanawake Bara msimu huu.
Kipa huyo aliitumikia Yanga Princess misimu miwili mfululizo na kipindi hicho hakupata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza tangu kocha Mzambia Charles Haalubono na sasa Edna Lema wainoe.
Chanzo kutokana Ruangwa Queens kimeliambia Mwanaspoti kuwa timu hiyo imemalizana na kipa huyo sambamba na mshambuliaji kutoka Fountain Gate, Irene Chitanda ikiwa ni sehemu ya kuimarisha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao. “Tumewaacha wachezaji kama wanne tuliokuwa nao katika mashi-ndano ya Ligi ya Mkoa tutaongeza baadhi ya wachezaji kwenye maeneo akiwemo huyo Adrophina na wengine ambao wana uzoefu wa ligi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Bado tuna muda mrefu wa kusajili asilimia kubwa tutaongeza wale wenye uzoefu na wachanga wachache ili watusaidie angalau kwa msimu huu tuusome kwanza kisha tutajipanga vizuri ujao.”
Huu ni msimu wa kwanza kwa Ruangwa Queens kuichezea Ligi ya Wanawake na ilipata nafasi hiyo baada ya kucheza mshindi wa tatu ikipokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Geita Queens.
Msimu huu timu zilizomaliza nafasi nne kwenye Ligi Daraja la Kwanza zimepanda moja kwa moja Ligi Kuu na kufikisha timu 12 badala ya 10. Timu hizo ni Ruangwa, Bilo Queens, Geita na Tausi wakichukua nafasi ya Mlandizi Queens na Gets Program zilizoshuka daraja.