BAADA ya kushindwa kufanya vizuri Dodoma Jiji na kutua Tabora United mshambuliaji, Reliants Lusajo ametaja sababu iliyomnyima rekodi ya upachikaji mabao msimu uliopita na kuahidi neema msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lusajo alisema hakuwa na msimu mzuri msimu uliopita kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara lakini anamshukuru Mungu msimu huu yupo fiti na ameahidi kuwa sehemu ya mafanikio katika kikosi cha Tabora United.
“Ni kweli sikuwa na msimu mzuri sababu ni majeraha, nashukuru kukaa kwangu nje kwa muda kumenirejesha kwenye utimamu nafikiri kama nitapata nafasi ya kucheza msimu huu wote nitakuwa na kitu cha kujivunia msimu ukiisha kwani nipo timamu na nipo tayari kwa ushindani,” alisema Lusajo na kuongeza;
“Nimefurahi kurudi kwenye ligi baada ya muda mrefu, hii inaniamsha kuonyesha ushindani kwani ukiwa nje kuna wachezaji wanafanya mambo mazuri na unasaulika kwenye ramani ya mpira ili niweze kurudi natakiwa kufanya maandalizi ya kutosha na kuonyesha ushindani naamini hilo litafanyika kwa uwezo wa Mungu msimu huu.”
Aidha nyota huyo anayeichezea pia Taifa Stars ameweka wazi malengo yake ni kuisaidia kufikia malengo, pia kumaliza ligi akiwa miongoni mwa washambuliaji waliotupia mabao mengi.
“Kufunga ndiyo kazi yangu siwezi kusema nitamaliza msimu bila kufanya hivyo ni mapema sana kuweka idadi ya mabao, lakini naahidi kila nafasi nitakayoipata nitaifanyia kazi ili kuwa sehemu ya washambuliaji bora, naendelea kuipambania timu.” alisema.