Mpina alikataa shangingi la INEC akiteuliwa kuusaka urais

Dar es Salaam. Wakati Mgombea urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina akiteuliwa rasmi kuwania nafasi hiyo, Chama hicho kimelikataa gari jipya aina ya Toyota LandCruiser GX VXR lililotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya kampeni za urais.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele, akizungumza leo Jumamosi Septemba 13, 2025 katika ofisi ndogo za INEC jijini Dar es Salaam baada ya kupokea fomu zake na kumteua, amesema magari hayo yanakabidhiwa wagombea wote wa urais ili kuhakikisha usawa katika kampeni.

“Tume imeamua kumpatia kila mgombea gari moja pamoja na dereva kwa matumizi ya kampeni,” amesema.

Hata hivyo, baada ya maelezo hayo, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Omar Shaban alisimama na kueleza kuwa chama hicho hakitapokea gari hilo.

“Kwanza tunashukuru sana kwa ukarimu mliotuonyesha, lakini tumependelea kutochukua gari. Tupo vizuri na tunaomba raslimali hiyo isaidie kwenye matumizi mengine,” amesema.

Akijibu kauli hiyo, Jaji Mwambegele amesema, “Sawa, ni mapenzi yenu. Lengo la magari haya lilikuwa ni kuweka usawa katika kampeni, lakini kama hamtalihitaji, tume italitumia kwa matumizi mengine.”

Hatua hiyo imekuja siku mbili tangu Mpina aliposhinda kesi dhidi ya INEC, kufuatia shauri la maombi ya kikatiba alilowasilisha kupinga hatua ya kuenguliwa kwenye mchakato wa uteuzi wa wagombea wa urais.

Agosti 26, 2025, INEC ilimzuia Mpina kurejesha fomu na kumwengua kwenye kinyang’anyiro hicho, hatua iliyomlazimu, kwa kushirikiana na Bodi ya Wadhamini ya ACT-Wazalendo, kufungua kesi dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake imewapa haki Mpina na Bodi ya ACT Wazalendo ikisema Katiba ilikuwa imekiukwa.