Dodoma. Benki ya Ushirika Tanzania na Shirika la Bima la Taifa (NIC) wamesaini makubaliano ya kibiashara ili kuyakatia bima mazao ya wakulima na wafugaji
Mkataba huo utadumu kwa miaka mitatu ingawa unaweza kuongezwa huku ukitajwa kuwa unakwenda kuwaondolewa hasara wakulima na wafugaji ambao kwa sehemu kubwa ndiyo wanufaika kwa benki hiyo.
Mkurugenzi wa Mtendaji wa Benki ya Ushirika, Godfrey Ng’urah amesema makubaliano hayo yatafaidisha wakulima na wafugaji takribani milioni 10 kupitia vyama vya msingi (Amcos) 6,000 vyenye wanachama milioni nane na Saccos 2,000 zenye wanachama milioni mbili.
“Makubaliano hayo yatawafikia wananchi asilimia 65 wanaojishughulisha na kilimo, mifugo, uvuvi hasa kwenye mnyororo wa kilimo-biashara ambao wanamiliki hisa za benki kwa asilimia 51,” amesema Ng’urah.
Mkurugenzi huyo amesema benki hiyo pamoja na kupata mkopo wa fedha za kukopesha wakulima na wafugaji kupitia Amcos na Saccos, wataikatia bima mikopo hiyo ili hata yakitokea majanga wanufaika wasipate hasara.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Abdi Mkeyenga amesema ushirikiano huo utajenga uchumi imara kupitia sekta ya fedha, ambayo inawafanya wakulima kuwa na uhakika wa kuvuna mazao kama walivyokusudia.
Mkeyenge amesema fedha inazokusanya NIC, watazitumia kuwekeza kwa kuikopea benki ya ushirika, ili iwakopeshe wakulima kupitia vyama vya msingi na Saccos
Taarifa zinaonyesha kuwa Benki ya Ushirika hivi sasa ina ukwasi wa Sh50 bilioni lakini utaongezeka hadi kufikia Sh100 bilioni ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, baada ya kukopa na kukopesha wakulima na wafugaji katika mnyororo mzima wa uzalishaji.
Meneja wa Bima Kanda ya Kati, Alex Sunzuguye amesema wataikatia bima mikopo kwenye maeneo matatu ambayo ni hali ya hewa, maeneo na mseto ya majanga, pamoja na magonjwa na moto.