Uvinza. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Kigoma kutumia fursa ya reli ya kisasa (SGR) inayojengwa mkoani humo kwani itakwenda kufungua biashara na uchumi wao.
Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa unatekelezwa katika awamu tofauti ili kuunganisha njia kuu za usafirishaji kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma na kuunganishwa na Burundi.
Hadi sasa, kipande cha kwanza cha Dar es Salaam – Morogoro na cha pili; Morogoro – Makutopora (Dodoma), tayari vimekamilika, huku vipande vingine vikiendelea kujengwa.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika Jimbo la Kigoma Kusini, leo Septemba 13, Samia amesema reli ya kisasa inatoka Dar es Salaam mpaka Kigoma, ikifika Uvinza inakwenda mpaka Msongati, Burundi, ambako itajengwa kwenda mpaka Afrika Kusini.
Amesema wamefanya hivyo ili wafungue njia za kufanya biashara, akieleza Bandari ya Dar es Salaam inashusha mizigo, inasafirishwa kwa reli mpaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Kigoma, hii ni fursa kubwa, hapa Uvinza bila shaka kutakuwa na kituo kikubwa cha reli hii, kwa hiyo ni fursa ambayo tunaomba mjipange muitumie kibiashara. Inakwenda kuifungua wilaya hii kwa kiasi kikubwa na inakwenda kukuza uchumi wa wilaya hii,” amesema.
Mgombea huyo amesema wataendelea kujenga miundombinu ya barabara na umeme katika mkoa huo ili kufungua fursa zaidi kwa vijana kujiajiri kwa shughuli mbalimbali za ujasiriamali ili kukuza uchumi wao.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, ambaye pia ni mratibu wa kampeni katika kanda ya Magharibi, amesema tangu Samia ameingia madarakani, amekuwa akihubiri amani na utulivu katika Taifa, kwani bila hiyo hakuna maendeleo.
“Msidanganyike na watu wanaotaka kuvunja amani yetu. Amani yetu ikivunjika hata maendeleo tunayoyatafuta hayatapatikana,” ameonya Pinda akizungumza kwenye mkutano huo.
Amewataka viongozi wa CCM kwenda ngazi ya chini kwenye mashina ili kukihakikishia chama hicho kinapata ushindi wa kishindo.

Vilevile, ameonya migawayiko ya waliotia nia, akisema mchakato wa kura za maoni ulikwisha na sasa wanatakiwa kuungana kukitafutia chama hicho kura.
Mgombea ubunge Kigoma Kusini, Nuru Kashakali maarufu Kandahali, amesema wananchi wilayani Uvinza watakwenda kumpigia kura Samia kwa sababu amefanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema Uvinza wamepata vituo vya afya vinne na chuo cha Veta na kilomita 54 za barabara kuanzia Uvinza hadi Ngurunga. Pia, amesema wamepata shule za msingi 34 na sekondari sita katika kipindi cha miaka minne ya Samia akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Katika jimbo letu kuna mradi mkubwa wa umeme wenye thamani ya Sh300 bilioni, hatukuwahi kuwa na mradi huo, lakini sasa unafanyika hapa katika Kata ya Kazuramimba,” amesema.
Amemwomba Samia awapatie barabara ya kutoka Simbo kwenda Karia, yenye urefu wa kilomita 300 ili kuwasaidia wananchi katika eneo hilo.
Pia, ameomba kwenye barabara hiyo wajengewe daraja ili kuunganisha pande mbili.