Tanzania, Kenya zaungana matumizi bora ya maji Mto Mara

Butiama. Nchi za Tanzania na Kenya zinatarajiwa kuwa na mpango wa pamoja wa matumizi bora ya maji ya Mto Mara, hatua ambayo itasaidia katika usimamizi na uendelevu wa mto huo, ambao hivi sasa unakabiliwa na changamoto nyingi hasa za uharibifu wa mazingira na kutishia uhai wake.

Kwa sasa tayari nchi hizo kila moja imeandaa mpango wake wa matumizi ya maji hayo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kunusuru mto huo na uharibifu unaoendelea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu.

Taarifa hiyo imetolewa wilayani Butiama Mkoa wa Mara leo Septemba 13, 2025 na Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la za Ziwa Victoria, Dk Renatus Shinhu wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya Mto Mara.

Amesema ofisi yake ndiyo imepewa jukumu la kuratibu uandaaji wa mpango huo wa pamoja na tayari majadiliano ya utekelezaji yameanza.

Dr Shinhu amesema lengo ni kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi wa pamoja katika kulinda na kuhifadhi bonde la Mto Mara ili liweze kudumu na kunufaisha wananchi wa nchi zote mbili kiuchumi na kijamii.

Amesema mpango huo utahusisha matumizi ya maji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, majumbani, kilimo, mifugo ambapo utawezesha nchi husika kutumia maji bila kuathiri nyingine pamoja na mto kwa ujumla.

“Mto Mara una umuhimu sana kwa ikolojia na bioanuai   ni muhimu kwa maisha ya watu na mazingira ambapo maji yake hutumika kwa ajili ya matumizi ya majumbani, mifugo, kilimo, madini pamoja na wanyama pori hivyo lazima tuwe na usimamizi kuhakikisha uendelevu wake,” amesema.

Amesema ili kuhakikisha mto huo na vyanzo vyake vinakuwa salama, hatua kadhaa zimechukuliwa ikiwamo za kisheria. “Watu watano  wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuvunja sheria za uhifadhi wa mazingira kwenye vyanzo vya maji.”.

Akifungua maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, amesema hatua mahususi zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha mto Mara unaendelea kuwepo na kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema umefika muda sasa matumizi ya maji ya mto huo yanafanyika kulingana na uwezo wa mto wenyewe ambayo itachangia katika uendelevu wake, huku akisema jamii zote kutoka Tanzania na Kenya zina wajibu wa kuutunza mto na kuhifadhi mazingira yake.

Akizungumza wakati wa upandaji miti na kusimika vigingi katika Kijiji cha Kirumi wilayani Butiama ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo ya 14 ya Mto Mara, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuhakikisha miti yote iliyopandwa inatunzwa.

“Hakuna sababu ya kupanda miti 8,000 halafu isikue hakikisheni mnailinda na kuitunza kwani   ina mchango mkubwa katika uhai wa mto wetu” amesema.

Amewataka wakazi wa vijiji vinavyozunguka bonde la Mto Mara kuheshimu mipaka iliyopo na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa.

“Tumesimika vigingi kuonyesha eneo la hifadhi, nawaagiza wananchi wote kuacha kuingiza mifugo na kufanya shughuli za kibinadamu katika eneo la hifadhi,” amesema.