Dar es Salaam. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema akipata ridhaa ya kuongoza dola, ataanza na marekebisho ya Katiba ili kuvifanya visiwa hivyo kuwa mikononi mwa Wazanzibari.
Othman ameahidi Wazanzibari watakuwa na uhuru wa kuhoji kuhusu mwenendo wa uendeshaji wa Serikali hiyo, kwa sababu Zanzibar ni nchi ya waungwana.
Amesema hayo leo Jumamosi Septemba 13, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni zake za kuwania urais zilizofanyika uwanja wa Tibirinzi, Chake Chake, Pemba.

“Hatuwezi kuendesha kwa misingi ya kikanuni na kijinga, kama ni kiongozi awe Rais, mwakilishi au diwani lazima apatikane katika misingi ya wazi, taratibu na awe amechaguliwa kweli na wananchi,” amesema na kuongeza:
“Akichaguliwa na wananchi watamuheshimu au siyo? Si Rais, mwakilishi au diwani akapatikana kwa njia isiyo halali na yeye akatafuta wengi wasiokuwa na uwezo wa kumuhoji.”
Othman amesema nchi haiwezi kuendeshwa kwa utaratibu huo, ndiyo maana ACT-Wazalendo inaeleza kuwa kazi yao ya mwanzo itakuwa kuirejesha Zanzibar mikononi mwa wananchi.
“Lazima turudi katika misingi ya kuendesha nchi kwa kuhakikisha kunakuwa na Katiba mpya, hii ndiyo ahadi yetu ya kwanza. Katiba mpya itakayojenga misingi ya uwajibikaji kwa kuwa na Tume Huru na mahakama huru,” amesema na kuongeza:
“Tukijenga misingi hii, Zanzibar itapiga hatua moja kusonga mbele, ndani ya Katiba Mpya tutahakikisha kunakuwa na vyombo huru vitakavyotoa haki. Tutahakikisha mahakama ipo huru na inayowajibika.”
Mbali na hilo, katika kudumisha maridhiano Zanzibar, watahakikisha kunakuwa na Tume Huru ya Maridhiano na Umoja wa Kitaifa ndani ya Katiba ya Zanzibar.
Amesema miongoni mwa mageuzi yatakayofanywa na chama hicho ni kuongeza mahakama maalumu ya kusimamia utawala kwa kila kiongozi, akiwemo waziri kufuata taratibu za kisheria za nchi.
Pia, Katiba mpya itaondoa urais usio na mipaka, akifafanua kuwa, wataweka utaratibu kuwa, Rais na makamu wake watakuwa na jukumu la kuwasimamia watakaopewa kazi.

“Kazi ya Rais itakuwa kuchagua majaji, waendesha mashtaka, mkaguzi wa hesabu za Serikali na taasisi zote zinazoisimamia Serikali. Hii ndiyo itakuwa kazi ya Rais, msimamizi na mlezi wa kuona mambo yatakwenda sawa, hizi nyingine za utendaji zitakuwa za Waziri Kiongozi,” amesema.
Othman amesema ataunda Serikali itakayotatua changamoto za wananchi kwa kuhakikisha wanakuwa na uwezo mzuri wa kiuchumi na kila mtu, akiwamo mkulima wa karafuu ananufaika na jasho lake.
Amesema Zanzibar imejengwa na karafuu, hivyo Serikali itakayoundwa na ACT-Wazalendo itaendeleza zao hilo kwa kuhakikisha wakulima wanapata haki zao ili kuimarisha kilimo hicho.
“Tunasema bado Zanzibar inaweza kusimama na kuzalisha karafuu ili kumwinua mwananchi, hakuna sababu ya kuwa maskini. ACT-Wazalendo itasimamia masilahi ya wananchi, Serikali nitakayoiongoza itamuhudumia mwananchi,” amesema.
Othman amesema: “Serikali tutakayoiunda itawezesha wananchi kiuchumi siyo kufanya usanii.”
Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, amesema Zanzibar haihitaji kukopa fedha ili kujiendesha kwa sababu ina haki na mamlaka yake kuendesha uchumi.
Amesema suala hilo ndilo atakalolifanya pindi atakaposhika madaraka kwa kuhakikisha Zanzibar inapata mamlaka yake kamili kuiwezesha kuendesha uchumi, pasipo kutegemea mikopo ili kisiwa hicho kisonge mbele.
“Kazi yetu ya mwanzo ACT-Wazalendo, Serikali tutakayoiunda na kuiongoza ni kumaliza changamoto hizi. Wao kwa miaka 60 yamewashinda, sisi kazi yetu ni kusimamia masilahi ya Zanzibar, ndiyo maana tunasema ni mwaka wa kuinusuru Zanzibar. Tunachokitaka ni haki za Zanzibar, hili ndilo jambo la kwanza, hatuwezi kuzitafuta bali zimeandikwa. Tutawaambia tu mkeka ndio huu, unaweza kukaliwa au kuondoa wote tukae chini,” amesema.