NRA waahirisha mkutano Tanga, sababu yatajwa

Tanga. Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), kimesema kimeshindwa kufanya mkutano wake ambao ilibidi ufanyike mkoani Tanga, kwa ajili ya kumnadi mgombea wake wa nafasi ya urais.

Akizungumza na Mwananchi mgombea urais kupitia NRA, Hassan Almasi ambaye ndiye katibu wa chama hicho leo Jumamosi Septemba 13, 2025 amesema wameshindwa kuendelea na mkutano wa Tanga kutokana na sababu za kiafya.

Amesema kwa sasa yupo mapumziko Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa muda akiangalia afya yake, hivyo hawataweza tena kuendelea na mkutano kwani kwa leo afya hairuhusu kupanda jukwaani.

Mgombea huyo amesema hawezi kuacha kuingia Mkoa wa Tanga kwa sababu kuna mgombea wao wa ubunge Handeni mjini, hivyo baada ya kupangwa ratiba toleo la tatu watafika mkoani Tanga kwa ajili ya kampeni.

“Nilipumzika Mwanga Moshi nikidhani asubuhi nitaamkia Tanga, lakini nimeamka afya yangu imekataa sipo vizuri kichwa kinasumbua na sauti, ila ratiba itakapokaa vizuri tutarejea Tanga kwa kuwa tuna mgombea wetu pale Handeni Mjini,”amesema Almasi.

Kwa mujibu wa ratiba ya wagombea urais iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), NRA ilitaka kufanya mkutano wake wa hadhara Tanga mjini, eneo la soko la zamani kuanzia saa mbili asubuhi mpaka 12 jioni.

Hali kama hii kwa mkoa wa Tanga ilitokea pia kwa Chama cha Alliance For Democratic Change, (ADC) ambacho kiliahirisha mkutano wake wa uzinduzi Tanga na kwenda kuufanyia mkoani Mwanza.