DK.SAMIA AUHUTUBIA MAELFU YA WANANCHI UVINZA AKIELEZEA MIRADI YA MAENDELEO

Na  Said Mwishehe,Michuzi TV-Uvinza

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM)Rais Dk.Samia SuluhHassa ameendelea kuchanja mbuga akisaka kura kuelekea Uchaguzi Mkuu ambapo leo Septemba 13,2025 amehutubia maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa Tambuka reli uliopo Kata ya Kazula Mimba wilayani Uvinza mkoani Kigoma Dk.Samia ameeleza yaliyofanyika miaka mitano iliyopita na    yale yatakayokwenda kutekelezwa miaka mitano ijayo iwapo watapata ridhaa.

Dk. Samia alisema mengi makubwa yamefanyika wilayani Uvinza huku akieleza Serikali imekamilisha ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Uvinza  na kuongeza idadi ya vituo vya afya na zahanati katika wilaya hiyo.

Pia, amesema Serikali imeongeza upatikanaji dawa kwa asilimia 11 ambapo sasa upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 91 wilayani Uvinza.”Kwa sasa hamuambiwi dawa mkanunue, dawa zote zinapatikana hospitalini. 

“Mkakati wetu tunapokwenda mbele na mkitupa ridhaa ni kuanza kwa majaribio utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote.Tukiweza vizuri mpango huo utafanyika kwa nchi nzima. Vilevile, tutajenga vituo vya afya vya Katanga, Kabengwa, Kasanza na kukamilisha ujenzi wa zahanati ambazo sasa zinaendelea kujengwa.”

Akieleza zaidi Serikali yake itakamilisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto huku akifafanua anatambua umuhimu wa kujenga kituo cha afya Kazuramimba kwa kuwa idadi ya watu imeongezeka na zahanati iliyopo haikidhi mahitaji.”Kituo hicho kitajengwa eneo la Kazurambimba.”

Kwa upande wa elimu, Dk.Samia amesema Serikali imeboresha mazingira ya kujifunza na kujifundishia.”Tumetumia zaidi ya Sh.bilioni 13 kuboresha elimu ya msingi ikiwemo ujenzi wa shule mpya za msingi 34 zilizowezesha kukidhi mahitaji ya udahili wanafunzi zaidi ya asilimia 100 ya lengo tulilojiwekea.

“Tulileta Sh.bilioni 19 zilizojenga shule za sekondari hivyo kufikisha idadi ya shule za sekondari 31,” amesema Dk.Samia alipokuwa akizungumza na wananchi wa Uvinza.

Akieleza zaidi Dk.Samia amesema kwa kutambua ujuzi kwa vijana, serikali imetenga Sh.bilioni 2.8 zilizokamilisha ujenzi wa chuo cha VETA pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia chuoni hapo.

Kadhalika, amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ikiwemo kukamilisha kituo cha walimu Uvinza.Pia, alibainisha kuwa serikali itaendelea na mpango wa kutoa elimu bila ada kuanz darasa la awali hadi sekondari.

Pamoja na hayo amesema ametoa  ahadi ya kuboresha mazingira ya kibiashara kwa kinamama wa kata hiyo ambao wamekuwa wakifanya biashara kando mwa barabara.