YANGA inaendelea kujifua tayari kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao Simba, utakaopigwa Septemba 16 na habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo kimataifa ni namna ambavyo wamerahisishiwa kazi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuikabili Wiliete Benguela ya Angola.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu wanatarajia kuanzia ugenini kwenye mchezo wao wa awali Ligi ya Mabingwa Afrika nchini Angola kati ya Septemba 19-21 na kumalizia nyumbani Tanzania Kati ya 26-28 Septemba 2025.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimelithibitishia gazeti hili kuwa wamepokea barua kutoka CAF ya kubadilishwa kwa uwanja ambao ulipangwa kuchezwa mchezo wao wa awali Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo awali ulipangwa uchezewe Benguela na sasa watakipiga Luanda.
“Tumepata unafuu kidogo mchezo wetu wa awali tutacheza mjini awali tulikuwa tukifika mjini tuanze safari nyingine kwenda kuutafuta Mji unaoitwa Benguela kwa ajili ya kwenda kucheza mchezo huo, sasa tumethibitishiwa kuwa utachezwa mjini ni faida kwetu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Kuna unafuu mkubwa mjini Luanda. Kwenda Benguela ni mwendo wa saa nane kwa usafiri wa gari lakini kwa usafiri wa ndege tulikuwa tutumie saa moja.”
Chanzo hicho kilisema uongozi na benchi la ufundi wamepokea kwa furaha taarifa hiyo na wanaamini itakuwa sehemu ya kunufaika kwao kwa kucheza kwa ubora bila uchovu kuelekea mchezo huo.
Wakati huo huo, Jumatatu alfajiri uongozi wa timu hiyo unatarajia kumtuma mmoja wa viongozi kuwahi Luanda kuandaa mazingira kwa ajili ya kuipokea timu siku moja baada ya kutoka kucheza dabi jijini Dar es Salaam.
“Mikakati inaendelea kufanyika wakati tunaendelea na maandalizi ya dabi Jumanne tuna mpango wa kumsafirisha kiongozi wetu mmoja Jumatatu.”