DP kuungana na CUF Uyole, mgombea awaita CCM na Chaumma

Mbeya. Wakati Chama cha Democratic Party (DP) kikitangaza kumuunga mkono mgombea ubunge Uyole, Ibrahim Mwakwama wa Chama cha Wananchi (CUF), mgombea huyo amesema matarajio yake ni vyama vyote kumnadi kutokana na kukubalika kwa jamii.

DP walitarajia kufanya mkutano wake wa kumnadi mgombea urais, Abdul Mluya mkoani Mbeya, lakini ziara hiyo haitakuwapo kutokana na dharura, badala yake nguvu waliyokuwa wameandaa wataielekeza kwa mgombea ubunge wa CUF, Mwakwama.

Mwakwama anatarajia kuzindua kampeni zake kesho Septemba 14 katika eneo la Makutano ya Uyole (Njiapanda), huku viongozi mbalimbali na wafuasi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla wakitarajia kuhudhuria kusikiliza sera za mgombea huyo.

Akizungumza leo, Septemba 13,2025 Katibu wa chama hicho, Osmeo Matheo amesema ratiba ilikuwa wawe na mkutano wa kampeni kumnadi mgombea urais wao, lakini kwa dharura iliyojitokeza, nguvu zote zitaelekezwa kwa mgombea ubunge wa CUF jimbo la Uyole.

“Kwa maana hiyo DP watakaokuwapo kesho tutamsapoti mgombea wa CUF jimbo la Uyole, tulitarajia sisi tuwe na mkutano wa urais Mbeya, lakini viongozi wamepata udhuru wakaghairi kuja” amesema Matheo.

Akizungumzia ugeni huo, Mwakwama amesema kutokana na kukubalika kwa wananchi, anatarajia vyama vingine vitampa nguvu kwenye uzinduzi huo, akieleza kuwa tayari amewatumia mialiko.

Mwakwama amesema hajagombea kwa bahati mbaya, bali anafahamu changamoto za wananchi wa Uyole na mwenye kuzitatua ni yeye, akiwaomba wote kwa pamoja kujitokeza kumsikiliza sera zake.

“Naamini wawe Chaumma, CCM, NCCR-Mageuzi, UPDP nao watakuwapo kama walivyofanya DP, hii inaonesha namna ambavyo nakubalika kwa vyama vyote na wananchi kwa ujumla.

“Kiuhalisia binafsi nayajua maisha ya wana Uyole, changamoto zote suluhisho ni mimi, niwaombe wajitokeze kwa wingi Njiapanda ya Uyole waje kunisikiliza mgombea wao kujua sera zangu” amesema mgombea huyo.

Amesema miongoni mwa sera zake ni kukabiliana na ubovu wa miundombinu ya barabara, maji na ajira kwa vijana akieleza kuwa iwapo wananchi watampa kura za ushindi, atahakikisha anawapa huduma hizo kwa ubora.