Mabinti wa Dhahabu wapewa heshima kwa kutwaa Kombe la Dunia

BAADA ya kufanikisha historia isiyosahaulika, wachezaji wa kike wa Tanzania waliowakilisha taifa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia kwa watu wasio na makazi, wamepatiwa pongezi za heshima.

Mashindano hayo yalifanyika Agosti mwaka huu nchini Norway, ambapo mabinti hao waliweka rekodi mpya ya kimataifa.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushiriki michuano hiyo kwa upande wa wanawake na iliwakilishwa na timu yenye wachezaji wanne kutoka kituo cha Future Stars Academy chenye makao yake Arusha, Moshi na Zanzibar.

Licha ya kuwa na idadi ndogo, mabinti hao walionyesha nguvu ya taifa baada ya kuwafunga mabingwa watetezi, Finland, kwa mabao 5-3 wenye mchezo wa fainali iliyopigwa jijini Oslo.

Kwa ushindi huo, wameweka rekodi ya taifa kuwa timu ya kwanza kupata taji la kimataifa katika mashindano maalumu ya Homeless World Cup kwa wasichana.

Mabinti hao wamefuata nyayo za timu ya taifa ya Tanzania kwa watoto wa mitaani wa kiume ambao mwaka 2014 walinyakua Kombe la Dunia kwa watoto wa mitaani, katika mashindano Street Child World Cup yaliyozishirikisha timu za mataifa mbalimbali duniani na kufanyika huko Rio de Janeiro, Brazil.

Meneja wa Future Stars Academy, Abel Mtweve, amewapongeza wachezaji hao kwa mafanikio hayo na kuweka wazi kuwa wataendelea kuhakikisha wanawashika mkono watoto wenye vipaji ambao hawana makazi na wale wanaoishi katika mazingira magumu.

“Kombe hili limepatikana kutokana na matunda mazuri ya wachezaji kwani tulienda na wachezaji wanne lakini wakapambana kuhakikisha ubingwa unarudi,” amesema Mtweve.

Aliongeza kuwa Future Stars Academy inashirikiana na Homeless World Cup kuendesha program za kijinsia na kutumia soka kuongeza uelewa juu ya changamoto mbalimbali za kijamii.

Kocha wa timu hiyo, Eva Mmary, ameeleza furaha kwa mafanikio ya wachezaji ambayo yametokana na upambanaji wake na ushirikiano mzuri ambao walipata kutoka kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Norway.

“Tulishiriki na wachezaji wanne tu kwa sababu ndio ilikuwa mara yetu ya kwanza kushiriki, mashindano hayo yanashirikisha wachezaji watatu ndani na kipa mmoja.”

“Tungependa kupeleka wachezaji wengi zaidi, lakini haya ndio yalikuwa mashindano ya kwanza ya kimataifa nje ya bara la Afrika tuliyoshiriki,” amesema Mmary.

Kocha Mmary aliongeza kuwa kushiriki mashindano ya Afrika mwaka jana jijini Arusha na Nairobi Kenya mwaka huu, kuliwasaidia wachezaji wake kuwa na ukomavu wa kimichezo.

Nahodha wa timu, Loyce Dismas, alikiri changamoto lakini akashukuru kwa ushindi, licha ya uchache na uchanga ila wakapambana na kurudi na ubingwa nyumbani.

“Tumefurahia kuona jitihada zetu zimerudi na medali, timu zenye majina makubwa zilitutia hofu, lakini kwa msaada wa Mungu na jitihada zetu, tulifanikiwa kumaliza kazi yetu,” amesema Loyce.

Kombe la Dunia la watu wasio na makazi ni mashindano ya kila mwaka ya soka kwa watu wanaokabiliwa na changamoto za ukosefu wa makazi au kutengwa na jamii, yanayoratibiwa na Homeless World Cup Foundation.

Mashindano haya hutumika kama ngazi ya mwanzo mpya, kusaidia kubadilisha maisha ya washiriki, kujenga mshikamano wa jamii, nidhamu, na maana ya maisha kwa wachezaji kutoka zaidi ya nchi 50.

Mechi zake hufanyika kwa muda mfupi, dakika 10 tu huku zikichanganywa na sherehe za furaha, na lengo kuu ni kusaidia kubadilisha mtazamo wa jamii kwa watu wasio na makazi na kuwawezesha wahusika kushiriki kikamilifu katika jamii.