Simulizi ya kijana aliyeuawa kikatili akituhimiwa kuiba parachichi

‎‎Iringa. Katika Mtaa wa Kisiwani, Manispaa ya Iringa, majonzi na simanzi vimetanda baada ya kijana, Yohana Mgaya, kuuawa kikatili kwa kupigwa na kisha kuchomwa moto akituhumiwa kuiba maparachichi.

Tukio hilo ambalo si tu limeacha majonzi kwa familia yake, bali pia kwa jamii yote ya Mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla lilitokea Septemba 11, 2025. Mwili wa Yohana ulizikwa Septemba 12.

‎‎Baba wa marehemu, Fredy Mgaya, ndiye aliyechoshwa zaidi kwa maumivu baada ya kupokea simu iliyomwarifu kuwa mwanaye amepigwa na kuchomwa moto na wananchi waliojichukulia sheria mkononi.

Baba wa marehemu Yohana Mgaya, kijana aliyefariki baada ya kupigwa na kuchomwa moto na kundi la watu waliomtuhumu kwa wizi wa maparachichi katika Mtaa wa Don Bosco, Manispaa ya Iringa. Picha na Christina Thobias



Akisimulia, tukio hilo baada ya Mwananchi kufika nyumbani kwake, Mgaya amesema Septemba 11, 2025 alipata taarifa kuhusu kuuawa mwanaye, akampigia simu mwenyekiti wa mtaa wake wa Kisiwani kuomba msaada wa haraka.

‎‎Mgaya amekana taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba kijana wake hakuwa na wazazi ikielezwa kuwa aliiba maparachichi ili kupeleka nyumbani kula na wadogo zake.

‎“Mtoto wangu alikuwa na familia, ninaishi naye na wadogo zake watatu. Si kweli kwamba alikuwa hana wazazi,” amesema akiwa mwenye uchungu.

‎Kwa sauti iliyojaa majonzi, Mgaya amesema hata kama kweli mwanaye alichukua maparachichi, haikuwa sababu ya yeye kupigwa hadi kufa na kisha kuchomwa moto.

‎‎“Ni tunda kweli ndiyo sababu ya kuondoa uhai wa mtoto,” amehoji Mgaya huku akibubujikwa machozi.

Ameeleza mwanaye Yohana alikuwa akisoma Shule ya Sekondari Mivinjeni, lakini alipofika kidato cha tatu aliacha akidai haelewi masomo.

‎“Nilijitahidi kumshawishi, lakini alikataa kabisa kuendelea,” amesema. ‎

Mgaya, amesema hakuna kinachoweza kufuta maumivu ya kumpoteza mwanaye.

“Nitamkumbuka daima kama kijana wangu, siyo mwizi wa maparachichi kama wanavyodai,” amesema.

Getrude Nyanyamba, jirani wa familia ya baba wa marehemu, Fredy Mgaya, akisimulia jinsi alivyomfahamu kijana Yohana Mgaya aliyepigwa na kuchomwa moto. Picha na Christina Thobias



Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisiwani, Twaha Witara amesema alipopata taarifa kuhusu tukio hilo la kusikitisha alikimbia kwenda eneo la tukio linalotajwa kuwa ni Don Bosco.

‎Mkazi wa Don Bosco ambaye hakutaka jina lake litambulike, amesema: ‎“Niliona mtoto akipigwa na kundi la watu wakimtuhumu kuiba maparachichi. Ilikuwa ni hali ya kutisha, kila mtu alikaa kimya akihofia kuingilia kati.”

‎‎Getrude Nyanyamba, jirani wa familia ya Mgaya ameeleza taarifa zilizosambazwa kuwa Yohana hakuwa na wazazi zilimsikitisha.

“Mtoto huyo alikuwa hana mama, lakini alikuwa na baba na wadogo zake watatu. Ni uongo kusema alikuwa yatima,” amesema.

‎ Jirani mwingine, Angel Keniku amesema jamii ya Kisiwani imepata somo kubwa kutokana na tukio hilo.

‎‎“Ni maumivu makubwa, lakini tunapaswa kuhakikisha tukio hili halijirudii,” amesema

‎Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ametoa tamko la onyo kali baada ya video ya tukio hilo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha mtoto huyo anavyopigwa na kina mama wawili kwa zamu kwa kutumia fimbo.

Akizungumza akiwa eneo la Don Bosco, alikemea vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi.

‎‎“Hatuwezi kuwa na jamii inayojichukulia sheria mkononi, hilo halikubaliki,” amesema.

‎James amesema Serikali haitavumilia vitendo vya kikatili vinavyohatarisha amani na kuhatarisha haki za binadamu.

‎‎“Tayari watuhumiwa wote waliokuwa wakihusishwa na tukio hili wametiwa mbaroni na wapo mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria,” amesema.

‎Ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla kuwa na imani na vyombo vya dola.

‎‎“Tukio hili la kinyama haliwezi kurudiwa iwapo kila mmoja ataheshimu sheria na kusubiri vyombo husika kuchukua hatua,” amesema.