Dk Shein: Dk Mwinyi ana uwezo mkubwa, Wazanzibari mpeni tena fursa

Unguja. Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Mohamed Shein, amemnadi mgombea wa CCM Dk Hussein Mwinyi kwamba ana uwezo mkubwa kuijenga Zanzibar, hivyo anastahili kuungwa mkono na kumchagua katika kipindi cha pili.

Dk Shein ametoa kauli hiyo leo Septemba 13, 2025 katika viwanja vya Mnazimmoja wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho, ambapo pamoja na mambo mengine amemkabidhi ilani ya chama hicho.

Dk Shein amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Dk Mwinyi ameiongoza Zanzibar kwa mafanikio makubwa na wala hakubahatisha, bali amepitia kwenye misingi ya ilani ya chama hicho.

“Dk Mwinyi anastahiki kupewa nafasi nyingine akafanye makubwa, maana uwezo wake ni mkubwa aliyoyafanya kwa kipindi cha miaka mitano anathibitisha hilo kwa kufanya kazi,” amesema.

Amesema hapana shaka Dk Mwinyi kasimama kidete kujitolea kusimamia umoja, mshikamano wa nchi na amekuwa akihubiri amani na kumtanguliza Mungu wakati wote.

Amesema katika uongozi wa miaka mitano wa Dk Mwinyi, amesimamia katiba zote ya Zanzibar na Tanzania na sheria bila kutetereka.

Amesema kuna miradi mikubwa ya maendeleo iliyofanywa ndani ya kipindi hicho ambayo ni ya kimkakati.

Amesema maendeleo huandaliwa, hupangwa na yanaletwa na fedha, kwa hiyo kukopa sio hila kikubwa ni maendeleo na wakubwa wote duniani wanakopa hata sisi tutaendelea kukopa na tutalipa.

Ameeleza kuwa katika awamu yake ya kwanza amejenga miradi mikubwa ambayo itazalisha ajira zaidi ya 25,000 yenye thamani ya Dola za Marekani 6.2 bilioni.

“Amewakomboa wanyonge, wenye kipato cha chini, maisha duni na kuwainua kiuchumi, ambapo ametoa mikopo 5,369 yenye thamani ya Sh39 bilioni.

“Haya sio mambo ya kubeza tunatakiwa kumuunga mkono na kumpa nguvu aifikishe Zanzibar mbali,” amesema.

Amesema ameanzisha harakati za uchumi wa buluu, licha ya watu wengi awali kubeza jambo hilo lakini ameonesha mafanikio makubwa katika sekta hiyo

“Niliwaambia CCM wenzangu wakati inaandaliwa ilani ya mwaka 2025 tuweke uchumi wa buluu, mwanzoni sikueleweka lakini mtaona kwa sasa mafanikio yake kutokana na jinsi Dk Mwinyi alivyoshughulikia,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Shein, viongozi waliotangulia walifanya sehemu yao, “kila mmoja amefanya kwa wakati wake na uwezo wake, Mwinyi ameendeleza na kufanya mengi.”

Amesema kuna ishu ya mafuta na gesi ambayo muda mrefu walikuwa wakitumia nadharia lakini ameonesha mafanikio makubwa na utafiti, ambao umeonyesha Zanzibar kuna mafuta na gesi nyingi chini ya ardhi na baharini.

Ameeleza mradi mwingine ambao watu hawakutegemea kama ungefanyika ni ujenzi wa daraja la Uzi ambalo tayari limeanza kujengwa likiwa na urefu wa kilomita 2.2.

“Ametawala Mreno zaidi ya miaka 250, Mjerumani karibia miaka 150 na Mwingereza, wote hao karibia miaka zaidi ya 400 lakini hakuna aliyeweza kujenga ila Dk Mwinyi katika kipindi cha miaka mitano kaonesha uwezo wake kalijenga,” amesema.

Awali Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha Rose Migiro akimkaribisha Dk Shein, amesema Zanzibar ya leo si ya miaka iliyopita yamefanyika makubwa.

“Ameendeleza ya watangulizi wake, kafanya zaidi, tunaamini akipewa ridhaa tena utaipeleka Zanzibar katika hatua nyingine kubwa ya maendeleo.”