Dar es Salaam. Kampuni ya mabasi ya Faima imetambulishwa rasmi na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kama mshirika wa kusafirisha abiria wa treni ya kisasa ya umeme (SGR) kwa mikoa ya Dodoma na Morogoro, hatua ambayo imeibua mitazamo tofauti kutoka kwa wadau wa sekta ya usafirishaji kuhusu ufanisi na athari za huduma hiyo.
Utambulisho rasmi wa kampuni hiyo umefanyika leo, Jumamosi, Septemba 13, 2025, mbele ya waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa TRC, Faima itaanza kutoa huduma zake kuanzia Septemba 15, 2025, kwa kuwachukua abiria wanaoshuka kwenye vituo vya Morogoro (Stesheni ya Jakaya Kikwete) na Dodoma (Stesheni Kuu Samia Suluhu Hassan), pamoja na kuwapeleka stesheni wakati wa kusafiri kwa treni ya SGR.

Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Maendeleo ya Biashara wa TRC, Frederick Massawe akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Septemba 13, 2025 jijini Dar es salaam.
Mabasi hayo ‘shuttle transport’ kwa Mkoa wa Morogoro yatatoa huduma ya usafiri kutoka Stesheni ya Jakaya Kikwete kwenda vituo vya Viwandani, Stendi ya Mabasi Msamvu, Masika na stendi ya zamani ya mabasi.
Kwa Jiji la Dodoma mabasi hayo yatatoa huduma ya usafiri kati ya Stesheni Kuu ya Samia Suluhu Hassan na kituo cha mabasi cha Nanenane, Machinga Complex na Shoppers Plaza na katika safari zote hizo nauli itakuwa ni Sh5,000.
Akizungumzia huduma ya mabasi hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Maendeleo ya Biashara wa TRC, Frederick Massawe amesema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa TRC wa kuboresha huduma za reli kwa kuzifanya kuwa jumuishi, bora, na zinazohusisha ushirikiano na sekta binafsi kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Taifa.
“Huduma hii mpya inalenga kuongeza urahisi wa usafiri kwa abiria wa SGR kwa kuwaunganisha moja kwa moja na mitandao ya barabara baada ya safari za reli. Tunaamini hatua hii itachangia na kuchochea maendeleo ya biashara na uchumi wa maeneo husika,”amesema Massawe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fahima, Ceaser Amin amesema katika utoaji huduma hiyo watakuwa na mabasi 13, kati ya hayo saba yatahudumia jiji la Dodoma na sita yatahudumia Mkoa wa Morogoro.

Mkurugenzi wa Fahima, Ceaser Amin akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Septemba 13, 2025 jijini Dar es salaam.
Amin amesema yapo yenye uwezo wa kubeba abiria 30 hadi 50 na watakuwa na uwezo wa kusafirisha abiria 472 kwa wakati mmoja kwa Dodoma na abiria 180 kwa Morogoro.
“Hata hivyo malengo yetu ni kuleta mabasi mengi zaidi ya haya huko mbeleni,”amesema Amin.
Walichosema boda, taksi mtandao, wananchi
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti kuhusiana na huduma hiyo, Katibu wa Chama cha Taxi Mtandao, Nobel Ford, amesema hilo lina faida na hasara kwao kwa sababu inaenda kutoa huduma kwenye mikoa ambayo wao wapo pia.
Kwenye faida, amesema huenda abiria akafaidika nayo kwa gharama kuwa chini ukilinganisha na yao waliokuwa wanatoza, huku akitolea mfano wa kutoka Stesheni Kuu ya Samia Suluhu Hassan kwenda stendi ya Nanenane sio chini ya Sh12,000 kwa gari.
Kuhusu hasara, amesema anaona madereva wanavyoenda kuathirika kwa kuwa anayetaka kwenda kwenye vituo vilivyotajwa kushusha abiria na mabasi hayo ni wazi hatahitaji huduma yao.
Pia, amesema hasara hiyo haitawaathiri madereva pekee bali pia Serikali, kwani mapato yatokanayo na kodi za maegesho na vibali kwenye stesheni huenda yakapungua, kutokana na madereva kulazimika kutafuta njia mbadala ya kupata abiria.

Ofisa habari wa Faima, Safina Abraham akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Septemba 13, 2025 jijini Dar es salaam.
“Abiria wengi wanapanda SGR hapa Dodoma ni wale wanaojiweza, na ndio maana unakuta anaachana na kupanda mabasi ambayo unaweza kutozwa nauli hadi Sh30,000 na kutokana na hilo ndio maana anaamua hata kuchukua usafiri binafsi, sasa kama kuna huu usafiri unakuja, ina maana watahamia huko,” amesema Ford.
Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma, Chacha Marwa amesema kwa faida anaona abiria watakuwa na uhakika wa kusafiri salama zaidi ukizingatia wengine huingia usiku, lakini pia kuepuka kuchelewa kwa kuwa mabasi hayo yatakuwa yanaenda kwa muda.
‘Ukiacha faida hizo lakini pia kwa watakaoendesha mabasi hayo kwao ni ajira na hivyo ule wimbo wa kuzalisha ajira nchini hapa sasa utakuwa unafanyika kivitendo,” amesema Marwa.
Katika ushauri wake, mwenyekiti huyo amesema pamoja na faida hizo ni vema kukawekwa utaratibu mzuri wa maegesho kwa mabasi hayo, bodaboda na bajaji ili abiria awe na uhuru wa kuchagua anataka kusafiri na chombo kipi.
Naye Mwenyekiti wa bodaboda na bajaji Mkoa wa Morogoro, Paul Sinya, amesema ujio wa usafiri huo kwao sio tishio, kwa kuwa hata taksi mtandao zilivyoanza ziliwakuta na wanaendelea kufanya nao kazi hadi leo.
Amesema bado usafiri wa boda na bajaji unahitajika, kwani hata katika vituo vilivyotajwa kuwa vitashusha abiria hao bado sio mwisho wa safari, wapo wanaoingia maeneo ya ndanindani hivyo lazima watahitaji huduma yao tu, lakini pia wapo wale wasiotaka kukaa kwenye foleni barabarani nao ni wapenzi wa usafiri huo.
“Kama haitoshi nauli ya bodaboda au bajaji huwezi kuilinganisha na usafiri mwingine na ni usafiri ambao watu wakishapanda wanaondoka haina kusubiriana,” amesema.
Baadhi ya wananchi wametoa maoni yao kuhusiana na hatua hiyo, ambapo Ashura Badi, mkazi wa Dodoma, amesema huduma hiyo itawarahisishia safari na kuongeza usalama, hasa kwa kuwa walikuwa wakitegemea zaidi usafiri wa bodaboda na bajaji, ambao si salama kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake, John Abdallah, mkazi wa Dar es Salaam, amesema hatua hiyo itanufaisha abiria wanaohitaji kuunganisha safari kuelekea mikoani, kwani hata wageni sasa hawatapata usumbufu, kutakuwa na usafiri wa uhakika kuwapeleka moja kwa moja stendi kuu za mabasi.