Mirerani. Madalali wadogo na wakati wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameiomba Serikali kutunga kanuni zitakazowawezesha kununua kila asilimia 20 ya uzalishaji wa madini hayo.
Hatua hiyo itawawezesha kufanyika magulio ya madini, pindi migodi ikizalisha tofauti na sasa inavyofanyika kwa hiari.
Baadhi ya madalali hao wadogo wameyasema hayo leo Septemba 13, 2025 kwenye gulio la madini ya Tanzanite lililofanyika ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini hayo kwenye mji mdogo wa Mirerani.
Ambrose Ndege, ameeleza kwamba endapo Serikali itaweka kanuni ya wazalishaji wa madini ya Tanzanite kuwauzia asilimia 20 ya madini yao wao nao watanufaika kiuchumi.
“Kuna baadhi ya wamiliki wa madini wenyewe wakizalisha madini wanauza kwa wanunuzi wakubwa kisha wanasafirisha nje ya nchi bila kupitia kwetu watu wa kati ili tufaidike hata kidogo,” amesema Ndege.
Ametoa ombi kwa Wizara ya Madini kutunga kanuni hiyo ya wazalishaji kuwauzia madalali wadogo asilimia 20 ya madini yaliyozalishwa Mirerani ili uchumi usambae kwa watu wa hali ya chini.
“Kuna migodi huwa inatoa madini ila madalali wa kati na wa chini hawapati chochote zaidi ya kutoa macho bila kupata chochote kitu,” amesema Ndege.
Soipey Koromo amesema suala la madalali wadogo na wa kati kupatiwa kipaumbele katika kuuza madini ya Tanzanite linapaswa kupewa msukumo.
“Sisi ni watu wa kati tunapaswa kunufaika na madini na siyo mtu anapata madini na kuuza kwa wanunuzi wakubwa,” amesema Koromo.
Mwenyekiti wa chama cha madalali wa madini Tanzania (Chammata) Jeremiah Kituyo, amezipongeza kampuni ambazo wameshirikiana nao kufanya magulio ya madini.
Hata hivyo, ameeleza kwamba wapo kwenye mazungumzo na kampuni nyingine ili nao watoe madini yao kwa ajili ya gulio la madalali wadogo na wa kati linalotarajiwa kufanyika wiki ijayo.