Mke wa diwani atokwa chozi la furaha akimnadi mume wake

Mbeya. Mke wa mgombea udiwani Kata ya Ruanda, Lydia Kibonde amejikuta akitokwa chozi la furaha wakati akimnadi mumewe, Isack Mwakubombaki na kutoa shukurani kwa wajumbe na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kumpitisha kugombea nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Lydia akizungumza leo Septemba 13, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni kwa mgombea huyo, amesema anawashukuru wajumbe na CCM ambao waliona mume wake anafaa kugombea nafasi hiyo, akiomba wananchi kumchagua ili kuwatumikia.

“Naishiwa maneno gani ya kusema zaidi ya kuwashukuru wajumbe na chama kwa ujumla kumpitisha mume wangu, sasa niwaombe wananchi kumpa kura nyingi Oktoba 29 ili akawatumikie wananchi,” amesema Lydia.

Kwa upande wake mgombea huyo, amesema iwapo atashinda udiwani atakuwa kiongozi mwenye kushirikisha wananchi kuleta mabadiliko katika Kata hiyo.

Amesema pamoja na hatua aliyofikia kupitishwa na chama kugombea, hawezi kubeza kazi ya waliotangulia kuongoza kata hiyo, akieleza kuwa ataendeleza walipoishia wengine.

“Kuna ambao niligombea nao lazima niwashirikishe kwa kuwa nao wana maono yao, nitaendeleza pale walipoishia wengine kwa kuwa kazi kubwa waliifanya,”amesema Mwakubombaki.

Mgombea udiwani Kata ya Iwambi, Grolia Ipopo ‘Mchina’, amesema Mwakubombaki ni moja ya wagombea bora mwenye uwezo, ushawishi na nguvu za kutumikia chama na wananchi.

Amesema kwa kazi alizoonesha kabla ya kupitishwa na chama, anaenda kufanya makubwa katika jamii akiwaomba wananchi kumpigia kura nyingi aweze kushinda.

“Ndio maana nimetoka Iwambi kuja kumpa sapoti kwa kuwa kazi yake tunaitambua, tunaomba kura nyingi kwa kijana huyu aweze kuiongoza Kata ya Ruanda,”amesema Mchina.

Mapema kada wa chama hicho, Tatu Mbamba amewaomba wananchi kutochanganya rangi za vyama akisema hata tochi haiwezi kufanya kazi kwa kuchanganya betri na gunzi.

“Chukua tochi uweke betri mbili na gunzi uone kama itawaka, ndio maana tunaomba kura kwa wagombea watatu wa CCM kuanzia udiwani, ubunge na urais ili waweze kufanya kazi vizuri,” amesema Tatu.