Watu 700 kutibiwa mtoto wa jicho Songwe

Mbeya. Zaidi ya wananchi 700 wakiwemo wazee waishio maeneo ya pembezoni mkoani Songwe, wanatarajia kunufaika na huduma uchunguzi wa mtoto wa jicho na upasuaji bure kwa lengo la kurejesha matumaini.

Kambi hiyo iliyoanza leo Jumamosi Septemba 13 mpaka 19 mwaka huu, itahusisha madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH) na Mkoa wa Songwe kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la Helen Keller International.

Mratibu wa Huduma ya Macho Mkoa wa Songwe, Dk Jofrey Josephat, ameiambia Mwananchi Digital leo Jumamosi Septemba 13, 2025 kuwa wamelenga kuhudumia wenye uhitaji ambao walishindwa kuzifikia huduma kutokana na ukata.

 Dk Jofrey ametaja baadhi ya sababu zinazochangia mtu kupata ugonjwa wa mtoto wa jicho kuwa ni pamoja na umri mkubwa, kisukari na mifumo ya maisha, lakini pia matumizi ya baadhi ya dawa ikiwamo steroid.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda, Dk Barnabas Mshangila amesema wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji, wana uwezekano mkubwa wa kurejesha matumaini na kuishi kama jamii nyingine.

“Tumejipanga kutumia muda mfupi kufanya upasuaji kwa teknolojia ya hali ya juu, ambayo mgonjwa hawezi kusikia maumivu kutokana na aina ya dawa atakayoitumia,” amesema.

Naye Meneja Mradi kutoka Shirika la Helen Keller, Athuman Tawakali amesema ujio wa huduma hizo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita kuboresha huduma za afya ya macho hususan kwa wananchi waishio maeneo ya pembezoni.

Amesema kambo hiyo imelenga kufanya uchunguzi wa afya ya macho na upasuaji bure kwa maelfu ya Watanzania waishio Mbeya, Songwe, Njombe na Iringa.

Naye Mkazi wa Songwe, Erica Mziho amesema miaka mingi amekuwa na changamoto ya macho na uoni hafifu, lakini ujio wa kambi hiyo ni kama mkombozi kwake.