KAMA ningetambua mapema kuwa mauaji yale yalifanywa na mwizi, nisingepata usumbufu wa kuificha ile maiti na kwenda kuitupa. Ningeripoti polisi na nisingepatwa na tatizo lolote.
Hapo hapo nikakumbuka kwamba mtu aliyeuawa alikuwa mume wa mtu, na aliuawa nyumbani kwangu usiku wa manane wakati mimi niliyekuwa naye ni mke wa mtu! Je, kama ningeripoti polisi, nini kingetokea? Nilijiuliza.
Bado yangekuwa matatizo, nikajijibu mwenyewe. Tatizo lingekuwa kushikwa ugoni. Na huenda polisi wangehitaji kufanya uchunguzi zaidi ili kujiridhisha kwamba ni kweli Shefa aliuawa na mwizi. Kama wasingepata uthibitisho huo, tatizo lingekuwa kubwa zaidi kwa upande wangu. Bora vile nilivyokwenda kuitupa ile maiti, nikajiambia.
Kwa kuona nilikuwa nimezorota mlo, nikapanga niende nikaoge kisha nitoke niende zangu saluni. Nikaenda kuoga. Nilipomaliza nilivaa na kutoka. Sikutoa gari; nilikwenda kukodi pikipiki ya bodaboda ili inipeleke saluni yangu.
Nilikuta wateja watatu waliokuwa wakishughulikiwa. Baada ya kusaliana na wafanyakazi wangu pamoja na wateja hao nilikwenda kuketi. Nilikaa hapo saluni hadi saa kumi na mbili jioni. Kiherehere kikanifanya nimpigie simu Raisa ili nijue kama alikuwa amempata huyo bodaboda wake aliyesema atamuulizia kuhusu namba ya usajili ya gari langu.
“Habari za saa hizi, shoga?” nikamsalimia alipopokea simu.
“Nzuri. Za huko?”
“Nashukuru, tunaendelea vizuri. Vipi, ulimuuliza yule kijana?”
“Kijana gani?”
“Yule wa bodaboda. Si uliniambia utamuuliza kuhusu namba ya gari ya yule mtu mliyemuona akitupa maiti kule makaburini jana usiku?”
“Ah… ndiyo. Yule kijana kila nikimpigia simu yake haipatikani. Nafikiri ipo kwenye chaji. Pale wanapoweka pikipiki zao wanaochajia simu zao.”
“Kwani kituo chake kiko wapi?”
“Kipo hapa Kwaminchi karibu na uwanja wa gofu.”
“Pale zinapokaa teksi?”
“Sasa, huu upande wa pili wa barabara.”
“Kwani anaitwaje yule kijana?”
“Anaitwa Mudi.”
Pia nilitaka nimuulizie namba ya simu ya kijana huyo, lakini nikaona Raisa atanishitukia. Nikabaki kumuuliza.
“Si utampigia tena baadaye?”
“Nitamjaribu usiku.”
“Sawa shoga; halafu kuna kitu nataka nikwambie…”
“Kitu gani hicho?”
“Unaonaje kesho tukaende kumfariji mwenzetu?”
“Mwenzetu nani?”
“Mke wa marehemu Shefa, angalau atuone tumefika kumpa pole.”
“Sawa. Tena nilitaka nikwambie: basi kesho nitakuja kwako twende.”
“Utakuja muda gani?”
“Nitakuja asubuhi.”
“Kabla ya kuja nipigie simu unijulishe.”
“Sawa. Nitakupigia.”
Nilipomalizana na Raisa nilipata wazo la kwenda Kwaminchi, kilipokuwa kituo hicho cha bodaboda, ili nimuone yule kijana anayetafutwa na Raisa kwenye simu. Nikampigia simu bodaboda wangu na kumuita. Baada ya robo saa hivi akawasili. Nikamwambia anipeleke Kwaminchi.
“Sawa. Kaa, twende,” akaniambia. Nikakaa upande wa nyuma ya siti, tukaondoka.
“Unakwenda Kwaminchi sehemu gani?” akaniuliza tulipokuwa tunakaribia eneo hilo.
“Nishushe popote tu,” nikamwambia.
Alinishusha karibu na kituo cha teksi cha Kwaminchi. Nilimlipa na nikatembea kwa miguu kuelekea kituo cha bodaboda alichonieleza Raisa. Nikavuka barabara kuelekea sehemu hiyo. Vijana wa bodaboda waliponiona wakaanza kunisonga, wakidhani nataka kuchukua pikipiki.
“Nina bodaboda wangu anaitwa Mudi,” nikawaambia.
“Mudi ametoka na mteja sasa hivi, unataka kwenda wapi?” kijana mmoja akaniuliza akiwa juu ya pikipiki yake.
“Nina shida binafsi na Mudi; sitaki bodaboda.”
“Labda umsubiri, au sema unakokwenda nikupeleke,” alisema mwingine.
“Nitamsubiri yeye,” nikajibu.
“Poa. Msubiri tu.”
Nikasubiri. Nilisimama hapo kama askari kwa karibu saa nzima, giza likinionyesha hisia. Baadaye nilimsikia yule kijana wangu akisema, “Mudi huyo anarudi.” Nilishukuru kwa kunitambulisha, kwani sikuwa namjua Mudi. Nikaona pikipiki ikiingia na kuegeshwa. Kijana huyo akashuka na kuelekea dukani.
“Mudi, kuna mgeni wako; anakusubiri,” yule kijana akamwambia.
“Acha tu, namfuata huko,” nikamwambia yule kijana kisha nikamfuata. Mudi alinisubiri.
“Unakwenda wapi?” nikamuuliza kama ningejua.
“Ninakwenda kuchukua simu yangu pale dukani. Niliiweka chaji muda mrefu.”
“Twende huko.” Nikafuatana nae kuelekea dukani.
Alipochukua simu aliiwasha kisha akaja pale nilipokuwa nimesimama. “Ndiyo, dada yangu, ulikuwa unasemaje?” akaniuliza. Wakati huo simu yake ikapigwa.
“Hebu subiri,” akaniambia. Alitazama namba ilimpigia kisha akipokea. Nilishituka niliposikia akisema, “Dada Raisa, vipi?”
Kwa kuwa sauti ya simu ilikuwa ya karibu, nilisikia mwanamke akisema, “Nimekuwa nikikutafuta tangu jioni; simu yako haipatikani.”
“Ilikuwa kwenye chaji, dada yangu. Ndiyo, nimeichukua sasa hivi. Wewe ndiye mtu wa kwanza unanipigia.”
“Nilikuwa nataka kukueleza kwamba yule mwanamke tuliyemfuata jana usiku makaburini, alikuwa anautupa mwili wa mtu ninayemfahamu.”
“Nimeshaisikia hiyo habari tangu mchana. Nilikuwa nakimbia bodaboda wenzangu hapa kwamba sisi tulimuona yule mtu akitupa huo mwili.”
“Wewe, si uliona namba za lile gari?”
Yule kijana akagutuka. Moyo wangu ukadunda kwa nguvu kwani suala la namba za gari lilinitia mashaka.
“Kwani ulitaka kufanya nini?” kijana huyo akamuuliza Raisa.
“Lile gari si linatafutwa na polisi?”
“Wewe si uliniambia unamfahamu mwenye gari lile?”
Moyo wangu ulizidi kupiga. “Ameniambia siye yeye; sasa mseme kweli, ni namba gani za gari? Kama umeziona hebu nitaje, kwani yule mtu ananihusu sana.”
“Huo ni ushahidi, dada yangu. Nilimueleza kaka yangu akaniambia nisijiingize tena katika suala hilo. Kama nimeona mwili ukitupwa basi ninyamze tu, nisije nikajitia matatizo.”
“Mambo gani tena hayo, Mudi? Si unitajie mimi tu?”
“Mimi naona tuachane na hizo habari, tusije tukajitia katika matatizo yasiyotuhusu. Unataka namba? Kesho unafuatwa, unauawa wewe…”
“We Mudi, mwoga sana. Atakayekufuata wewe akuue ni nani?”
“Binaadamu. Wewe hujui yule mtu ameuawa na nani na kwa sababu gani.”
“Kama unaogopa kuongea kwenye simu nitakutafuta kwa muda wangu uniambie.”
Simu ya upande wa pili ikakatwa. Mudi akaiweka simu mfukoni. “Ennhe… ulikuwa unasemaje?” akaniuliza.
“Kwanza nipe namba yako. Siku nyingine nikikuhitaji nisipate tabu.”
Yule kijana akanitutumia namba yake, nikaihifadhi kwenye simu yangu kisha nikampigia ili apate namba yangu.
“Niandike jina gani?” akaniuliza baada ya namba yangu kutokea kwenye simu yake.
“Andika Susana,” nikamtajia jina la mfanyakazi wangu.
Alipoandika nikamwambia, “Nataka unipeleke Mikanjuni.”
“Mikanjuni sehemu gani?”
“Katika ule mtaa ulikotokea msiba wa yule mtu aliyeokotwa makaburini leo asubuhi.”
Mudi akanitazama kwa makini. “Ahaa… mimi siufahamu huo mtaa.”
“Si nimesikia ukizungumza kwenye simu?”
“Umenisikia nimezungumza nini?” yule kijana akanikazia macho; alionekana muoga kweli.
“Si nimekusikia ukizungumzia kuhusu mtu aliyeuawa na kutupwa makaburini jana usiku.”
“Lakini huo mtaa wenye msiba siufahamu.”
“Kumbe huyo mtu alipokuwa anatupwa uliona?”
“Unajua, jana usiku kuna mwanamke mmoja nilikuwa nampeleka safari zake. Akamuona huyo gari akaniambia nilifuate. Nikalifuata hadi Msambweni. Sasa kule alishuka kwenye pikipiki akalifuata lile gari. Baadaye gari lako likarudi na kuondoka; yeye akatuja kuniambia twenzetu. Sasa mimi sikujua kilichotokea.”
Kijana huyo alikuwa ameshageuza maneno; alivyosema simu vilikuwa tofauti na alivyonieleza.
“Kwa hiyo wewe hukuona yule mtu akitupwa?” nikamuuliza.
“Labda yeye aliona.”
“Na hizo namba za gari hukuziona?”
“Zinanihusu nini? Mimi niko kwenye kazi yangu.”
“Basi nipeleke huko Mikanjuni,” nikasema.
“Wewe mwenyewe si unapafahamu?”
“Nitauliza watu huko.”
“Sawa, twende.”
Wakati tunaenda kwenye pikipiki aliniuliza, “Kwani huyo mtu aliyeuawa ni nani wako?”
“Mke wake ndiye ninayefahamiana naye,” nikamjibu.
Kijana huyo hakuniambia kitu tena.
Inaendelea…
Bado Watatu – 28 | Mwanaspoti
