Sasa Kipigwe! Ecua apagawa, Simba kambini kunapikwa

SASA kipigwe! Hicho ndicho unachoweza kusema baada ya Simba na Yanga kumaliza ratiba za matamasha yao yaani Simba Day na Wiki ya Mwananchi mtawalia, huku kila upande sasa ukijifungia kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa keshokutwa, Jumanne, Septemba 16.

Simba ndiyo walioanza kuliamsha na Simba Day Jumatano, Septemba 10 wakifuatiwa na watani wao, Yanga waliokuja na kilele cha Wiki ya Mwananchi, ambapo mastaa kibao wa pande zote waliosajiliwa msimu huu na waliokuwapo uliopita wakikiwasha kwenye Uwanja wa Mkapa na kushinda dhidi ya wapinzani wao, timu mbili kutoka Kenya Gor Mahia na Bandari.

Simba ilianza kuonyesha kikosi chake na kuifunga Gor Mahia mabao 2-1 huku Yanga ikiilaza Bandari bao 1-0 na hivyo kuhitimisha wiki kadhaa za maandalizi kwa ajili ya matamasha hayo ya kila mwaka.

Baada ya matamasha hayo yaliyoambatana na burudani za aina mbalimbali, hivi sasa kila upande umejifungia kupangilia mambo kwa ajili ya dabi ya kwanza ya Kariakoo msimu huu ambapo wababe hao watakipiga kuwania Ngao ya Jamii, mechi inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa pande zote; na hivyo sasa kipigwe tu!

Mastaa wapya wa Yanga wamekiri kuwa hitimisho la Wiki ya Mwananchi limewaachia deni kubwa la kuifanyia klabu hiyo wakitoa ahadi kwa mashabiki, huku Celestine Ecua akisema: “Huu ni mwanzo tu mabao mengi yanakuja.”

Yanga ilitambulisha mastaa 30 watakaoitumikia msimu huu wa 2025/26 na baada ya utambulisho juzi ilipocheza dhidi ya Bandari ilishinda 1-0 kwa bao lililofungwa na kiungo mshambuliaji, Ecua.

Miongoni mwa mastaa wapya waliozungumza na gazeti hili ni mchezaji huyo aliyetua Yanga akitokea Asec Mimosas aliyesema: “Nilitaka kumuomba kocha niendelee kuwa uwanjani, lakini niliona umuhimu wa wenzangu kucheza. Bahati nzuri nilikuwa nimefunga bao kwenye mechi yangu ya kwanza mbele ya mashabiki.


“Kweli kabisa nataka kuendelea kufunga na sasa nataka kuendelea kufunga hata kwenye mechi ijayo ili kuendeleza furaha ya mashabiki wa Yanga ambao wameonyesha mapenzi yao kwa timu.”

Naye Lassine Kouma, mrithi wa aliyekuwa kiungo mkabaji wa Yanga, Khalid Aucho aliyetimkia Singida Black Stars alisema anaamini yupo katika timu kubwa na hakuwahi kukutana na mashabiki wengi kiasi kile.

“Sijawahi kucheza mechi yenye mashabiki wengi vile. Hata klabu nilizochezea japokuwa nilikuwa naambiwa na wenzangu jinsi timu moja inavyoweza kujaza uwanja mkubwa kama ule,” alisema Kouma ambaye ni raia wa Mali.

Beki Mghana Frank Assinki alisema: “Kwa namna mashabiki wa Yanga walivyokuwa wanashangilia uwanjani juzi, nilijiona ni kama naongezeka nguvu kutokana na mzuka. Walichofanya uongozi na mashabiki ni kama deni ambalo tunapaswa kulilipa msimu huu kwa kuwapa mafanikio kuchukua makombe. Ukweli ni kwamba timu ya kuchukua makombe tunayo. Zipo timu za kutupa changamoto, lakini sio kuzuia mafanikio.”


KOCHA wa Simba Fadlu Davids amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo katika mchezo dhidi ya Yanga akisema kuwa kikosi hicho kitakuwa na mabadiliko makubwa, huku mabosi wa klabu hiyo wakikutana katika kikao kizito cha kujadili mambo makubwa mawili.

Tayari Simba imerejea kambini jana kujiwinda na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga unaotarajiwa kupigwa keshokutwa, Jumanne kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema amesikia mengi juu ya matamanio ya mashabiki na viongozi katika kuboresha kikosi na yote ameyachukua akiyafanyia kazi hivi sasa.

Fadlu alisema kuwa anafahamu mchezo unaofuata sio mwepesi kwani Simba inakwenda kukutana na timu yenye mastaa wenye uwezo ambao hawapaswi kuchukuliwa poa.

“Simba inarudi kambini kuendelea kujipanga na mchezo wa Ngao ya Jamii, ambayo ninaamini tutakuwa sawa ingawa tunakutana na timu kubwa – Yanga, hivyo lazima maandalizi yetu yawe ya kutosha.”

Alisema watapata matokeo baada ya muda mfupi kwani anajua kwamba bado kuna kazi inatakiwa kuendelea kufanyika hasa kuboresha eneo la mbele la ushambuliaji.

“Najua kiu ya Wanasimba wengi ni kuona timu inakuwa imara kwenye kila eneo kutokana na michuano ambayo iko mbele yetu na kutimiza malengo ya klabu. Kwa sasa nimeanza na maboresho ya eneo la mbele baada ya muda mfupi kile ambacho wengi walikilalamikia kitakuwa kimepata ufafanuzi,” alisema Fadlu.


Aliongeza kuwa: “Simba ni timu kubwa ambayo inatakiwa kuendelea kuimarishwa taratibu, lakini haikuwa rahisi kuonyesha nguvu yetu kubwa kwenye mchezo wa kirafiki badala ya kuangalia malengo makubwa yaliyo mbele.”

Jana, Mwanaspoti lilielezwa na chanzo kimoja ndani ya Simba kwamba imeitisha kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ambacho kitajadili mchezo dhidi ya Yanga na ule wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana.

Simba itakutana na Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii keshokutwa na baada ya hapo itasafiri kwenda Botswana ambako itacheza Jumamosi, Septemba 20.