JKT, Polisi nusu fainali ya kibabe

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Cecafa kwa wanawake, JKT Queens Septemba 14 saa 9 jioni kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi, Kenya itakuwa na kibarua cha kufuzu fainali ya michuano hiyo ikiivaa Polisi ya Kenya.

Kabla ya mechi hiyo itatanguliwa na nusu fainali ya kwanza kati ya Rayon Sports Women ya Rwanda na Kampala Queens ya Uganda.

Bingwa wa michuano ya Cecafa ndiye atakayewakilisha ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwenye mashindano Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake itakayofanyika mwezi ujao nchini Algeria.

JKT ilifuzu hatua hiyo baada ya kumaliza kinara wa kundi C ikikusanya pointi sita ikiwa haijaruhusu bao huku ikitikisa nyavu za wapinzani mara saba, ambapo mechi ya kwanza iliichapa JKU Princess kwa mabao 5-0 na 2-0 dhidi ya Yei Joints ya Sudan Kusini.

Wenyeji Kenya Polisi walifuzu nusu fainali wakimaliza kileleni mwa kundi A kwa pointi sita, wakishinda 1-0 dhidi ya Kampala Queens kisha kuichapa Denden 2-0.

Hii ni mara ya kwanza mabingwa hao mara nne wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania kukutana na wenyeji hao ambao ni mara ya kwanza kushiriki Cecafa.

Kocha msaidizi wa JKT, Azishi Kondo alisema walitamani kukutana na timu hiyo akiamini mechi hiyo itatoa taswira ya ubora wao kimataifa.

“Polisi ni mabingwa hapa Kenya. Tulitamani kukutana nao na imekuwa hivyo, malengo yetu ni kuonyesha mechi nzuri, lakini kufuzu hatua ya fainali na tuwe mabingwa ingawa haitakuwa rahisi,” alisema Kondo.