Dar es Salaam. Kila mmoja atakubaliana na mimi kwamba uhusiano baina ya wapendanao ulikusudiwa kuwa wa upendo, maelewano, kuaminiana, na urafiki wa hali ya juu.
Kwa bahati mbaya hali halisi siyo hiyo katika uhusiano wa watu wengi. Wengi wetu tumeumizwa kwa mpenzi mmoja au mara nyingine wote kutokuwa waaminifu katika uhusiano.
Kutokuwa mwaminifu hapa namaanisha hali ya mpenzi mmoja kuwa na uhusiano usio rasmi na mpenzi au wapenzi wengine pembeni.
Japo jambo hili hufanyika kwa siri sana kwa kuogopa kuharibu uhusiano mtu alionayo, wako baadhi ambao wamegundulika na uhusiano ukaathirika kwa kiasi kikubwa na wengine ulikufa kabisa.
Wako ambao wameweza kuhimili machungu ya kugundua hali ya wapenzi wao kutokuwa waaminifu lakini pia wako ambao imewashinda kabisa kuwa wavumilivu, wako ambao hali hii imewaletea shida kihisia, kisaikolojia na hata kiafya.
Kwa bahati mbaya wengi wetu hatuzijui hata dalili au alama zozote za kutujulisha mabadiliko waliyonayo wapenzi wetu ili basi angalau tuanze mapema kufanya uchunguzi au kupeana tahadhari kabla makubwa na machungu zaidi hayajatokea. Zifuatazo nia alama zitakazokusaidia kuwa macho mara utakapoona mazingira ya kufanana nazo yanatokea katika uhusiano wenu.
Alama hizi nimezikusanya katika mazungumzo na baadhi ya watu niliowahi kusaidiana nao kutatua matatizo ya uhusiano na pia nikazihakikisha kupitia kusoma vitabu mbalimbali, kwahiyo nina uhakika zitakusaidia kuona uhalisi wa mambo, na yumkini utaona baadhi ya alama ambazo umeshawahi kuzihisi au kuzishuhudia katika uhusiano wako.
Kuongezeka ghafla kwa hali ya kujipenda
Yawezekana mpenzi wako alikuwa amezoea kuvaa kawaida, hapa simaanishi kutopendeza, na wewe ulikuwa umemzoea katika hali fulani ya mavazi au mitindo mara ghafla anabadilika na kuwa mtanashati zaidi, ana badilisha mavazi, anapenda mavazi ya gharama, labda alikuwa hatumii manukato lakini ghafla anaanza kupenda manukato tena ya gharama.
Anakuwa mtu wa kujijali zaidi ya kawaida yake kiasi ambacho hukumzoea. Katika hali hii jaribu kuwa macho zaidi kufahamu nini kilichosababisha mabadiliko ya ghafla kiasi hicho.
Kuanza kuchelewa kutoka kazini mara kwa mara
Sio kwamba kila mtu anapochelewa kutoka kazini basi anakuwa sio mwaminifu, lakini zaidi ya asilimia 75 ya ambao wamekuwa na uhusiano nje wamekuwa wakitoa visingizio vinavyohusiana na kazi, vikao, mikutano na safari za kikazi. Wewe ni shahidi wa hili.
Unaweza kukuta mtu alikuwa anafanya kazi hiyo muda mrefu tu tangu muanze mapenzi yenu, mara ghafla hali inabadilika, siku hizi anachelewa sana kurudi nyumbani, na anaporudi unaweza kutegemea utamwona amechoka kimwili na hata kiakili kwa majukumu ya kazi kuhusiana na asili ya kazi anayoifanya lakini unakuta mtu wala haonyeshi kuchoka, ana furaha kama kawaida.
Hali hii inapojitokeza mara kwa mara usichelewe kufungua macho na kudadisi mazingira maana, ni kweli amepata kazi ya ziada ila siyo ile ya ajira unayoijua wewe.
Kupenda kutembea na mipira ya kinga mara kwa mara
Inashangaza mara nyingine kusikia mpenzi mmoja ana tabia ya kubeba kondom kwenye pochi yake au mfukoni kwa kisingizio kuwa anajali, cha kushangaza zaidi unakuta yuko katika uhusiano na mkewe au mumewe.
Yumkini ni kweli kuna kujali na labda katika uhusiano yenu hili sio la kushtua kwa sababu mnajali afya zenu au mnatumia kondomu kwa sababu zaidi ya moja, lakini inakuwaje pale unapogundua kuwa ile kondom uliyokuwa unaiona haipo tena hukuhusika katika kuitumia.
Mazingira tatanishi ya simu
Inawezekana mpenzi wako sio mtu wa kupokea simu au kupiga simu sana, na hivi ndiyo ulivyomzoea, mara ghafla simu zinaanza kumiminika mpaka muda wa usiku.
Inawezekana pia alikuwa yuko huru hata simu yake inapolia unaweza kuichukua na kumpatia lakini ghafla anakuwa na hofu kubwa na kuificha simu yake.
Nimeongea na wengine ambao wanakwenda na simu hadi bafuni isije ikasikika. Wengine wameanza kuondoa milio katika simu zao wakati haikuwa kawaida yao, wako ambao simu zao zikipigwa hawawezi kuzipokea na kuongea kwa uhuru kama kawaida.
Ataondoka na kujitenga pembeni akijifanya anaongea kiuaminifu kabisa lakini mtu uliyempenda na umkamzoea unaweza kugundua uhalisi wa anachokiongea kwenye simu na jinsi ya anayeongea naye kwa kumuangalia usoni tu.
Yumkini mpenzi wako amepigiwa simu na kwasababu hakuwepo karibu ukaipokea, na mara mpigaji wa simu anapogundua aliyepokea sio mwenye simu, anakata simu hiyo ghafla.
Au unagundua kila simu inayopigwa kwenye simu ya mpenzi wako haionyeshi namba au haionyeshi jina. Mazingira kama haya yanapozidi basi jaribu kuchukua hatua, inawezekana kuna mvamizi tayari katika uhusiano wenu.