Wananchi Kigoma waeleza matumaini yao kwa mgombea urais wa CCM

Kigoma. Wananchi wa Kigoma wameeleza matumaini yao kwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, wakimtaka atekeleze ahadi alizozitoa kwenye huduma mbalimbali za kijamii.

Wananchi hao wameeleza hayo kwa nyakati tofauti leo Sepemba 14, 2025 kwenye mikutano ya kampeni ya mgombea huyo wa urais, ambayo ameifanya katika majimbo mbalimbali mkoani humo ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake.

Kigoma ni moja ya mikoa ya pembezoni ambayo kwa kipindi kirefu iliachwa nyuma, hasa katika huduma za jamii na miundombinu, jambo ambalo limeufanya mkoa huo kubaki nyuma kimaendeleo.

Hata hivyo, Serikali ya awamu ya sita imeufungua mkoa huo na kuufanya kuwa unaofikika kwa urahisi, huku mradi wa reli ya kisasa (SGR) ukitarajiwa kuleta mapinduzi makubwa siku zijazo.

Mkoa huo kuunganishwa na gridi ya Taifa kumechangia kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme wakati wote na kuongeza uwekezaji wa viwanda mkoani humo.

Wakizungumza na Mwananchi, wananchi hao wameeleza mabadiliko yaliyofanyika katika jamii zao, huku wakitaka akatekeleze mengine aliyowaahidi kwenye maeneo yao.

Hillary Kiiza, mkazi wa Kigoma mjini, amesema angependa kuona mgombea wa CCM aongeze upatikanaji wa maji wa uhakika katika mji huo ili wananchi wafurahie huduma hiyo wakati wote.

Pia, amesema huduma za afya kwa bima kwa wote zitekelezwe ili wananchi wasio na uwezo wapate matibabu bila kudaiwa fedha nyingi ambazo hawawezi kuzipata, ili kuokoa maisha yao.

“Nilimsikia mama akisema atatoa matibabu bure kwa wasio na uwezo. Hizo ni habari njema hasa kwa sisi wananchi wa chini tusio na fedha za kujitibia. Tunaomba Mungu amsaidie akatimize hiyo ahadi yake ili nasi tuguswe,” amesema Kiiza.

Mkazi wa Kasulu, Hamis Buyanga, amesema changamoto kubwa katika mji huo ni barabara za lami, ambazo zitasaidia kupunguza vumbi na kuupendezesha mji huo.

“Nimemsikia mgombea wa CCM akiahidi kujenga barabara hapa Kasulu, nina imani atatekeleza, kwa sababu hata hizi chache tulizonazo ni yeye ndiye ametujengea. Naomba akatekeleze na hizo nyingine alizoahidi ili mji wetu upendeze,” amesema kijana huyo.

Kwa upande wake, Amina Masoud, mkazi wa Uvinza, amefurahishwa na ujio wa Samia katika wilaya hiyo kwani alikuwa na hamu ya kumuona. Ameeleza matumaini yake kwa kiongozi huyo, kwani ameshuhudia maendeleo makubwa yaliyofanyika katika kata yake ya Kazuramimba.

“Mama Samia ni mwanamke, anajua kero zetu wanawake hasa kwenye huduma za uzazi. Tunashukuru ametujengea kituo cha afya hapa Uvinza, sasa tunajifungua vizuri, hauendi mbali kama zamani. Tunaomba atuangalie na kwenye barabara, tupate soko ili tufanye biashara vizuri,” amesema mwanamke huyo.

Kada wa CCM Kigoma mjini, Yusuph Hamza, amesema mwenyekiti wao ni kiongozi makini wanayeamini atatekeleza ilani ya CCM kwa asilimia 100, hususan kwa Mkoa wa Kigoma ambao anataka kuufanya kitovu cha biashara.

“Jana mlimsikia akisema ataufanya Mkoa wa Kigoma kuwa kitovu cha biashara. Sisi hatuna wasiwasi naye, kazi amefanya, kazi atafanya. Oktoba 29 tunakwenda kumrundikia kura za ushindi,” amesema.