Wananchi wa Kalila walia zahanati kutokamilika

Rukwa. Wananchi wa Kijiji cha Kalila, Kata ya Kabwe, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, wameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho, ambayo imeshindwa kukamilika kwa muda mrefu sasa.

Wamesema kutokana na kadhia hiyo, wajawazito hujikuta wakijifungulia njiani au majini wakiwa kwenye mitumbwi wakifuatilia huduma hiyo katika maeneo mengine.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Septemba 14, 2025, katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu za udiwani uliofanyika kijijini hapo, baadhi ya wananchi akiwamo Ramadhani Masesa, wamesema hali hiyo ni fedheha kwa utu wa binadamu.

“Ni aibu kubwa mjamzito kujifungulia njiani au kwenye mtumbwi. Shangazi yangu aliwahi kujifungulia mikononi mwangu tukiwa majini ndani ya boti. Nililazimika kumsaidia wakati mimi si mume wake. Tunaomba wahusika watusaidie, ni haki yetu kuwa na zahanati,” amesema Masesa.

Amesema changamoto kubwa wanazokumbana nazo ni ukosefu wa huduma za afya na miundombinu duni ya barabara, hali inayochangia usumbufu mkubwa, hasa kwa wajawazito na watoto.

Masesa amesema licha ya jitihada za kushirikiana na viongozi wa kijiji chao, maendeleo ya msingi kama barabara na zahanati yamekuwa yakisuasua kwa miaka mingi.

“Viongozi mbalimbali wamekuwa wakitoa ahadi zisizotekelezeka. Sisi si wanyama. Kinamama kujifungulia majini mbele ya watoto wao ni hali isiyokubalika kabisa,” amesema mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Merry Deserio.

Kijiji cha Kalila kipo mwambao wa Ziwa Tanganyika, na ili kupata huduma za afya, wananchi wanalazimika kupanda boti au mitumbwi, jambo linalowapotezea muda na kuhatarisha maisha yao.

Katibu wa CCM Wilaya ya Nkasi, Anastasia Amos, aliyeshiriki mkutano huo, amesema chama kimepokea maombi ya wananchi na kuahidi kuyafanyia kazi endapo kitapata ridhaa ya kuongoza Serikali.

“Makosa yaliyofanyika miaka mitano iliyopita hayatarudiwa. Ingawa siyo sababu ya kukosa zahanati, tukipata ridhaa ya kuongoza jimbo hili la Nkasi Kaskazini, tutahakikisha changamoto hii inaondoka,” amesema Amos.

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Kabwe, Sebastian, amewaomba wananchi kumpa ridhaa ili aendeleze alipoishia mtangulizi wake, aliyefariki dunia miaka miwili iliyopita.

“Mkinichagua mimi na mgombea ubunge, tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha kero hizi tunazitatua,” amesema mgombea huyo wa udiwani.

Mgombea ubunge wa Nkasi Kaskazini, Salum Kazukamwe, akizungumza kwenye kampeni hizo, ameahidi kushughulikia changamoto za wananchi hao, akisema kipaumbele chake kitakuwa kukamilisha ujenzi wa zahanati na kuboresha barabara.

“Nikipewa ridhaa ya kuongoza, nitahakikisha wananchi wanapata huduma za afya na changamoto za barabara zinashughulikiwa.

“Kutokana na hali ya sasa, mazao yenu yamekuwa yakiharibiwa na wanyama pori kwa sababu hakuna miundombinu ya barabara inayowawezesha kuyafikisha sokoni. Nitashughulika na hili kwa dhati,” amesema Kazukamwe.