BAADA ya kuitumikia Coastal Union kwa msimu mmoja, straika wa Kitanzania, Mgaya Ally amesema ni muda wa kuendelea kutafuta changamoto sehemu nyingine akitimkia Salalah SC ya Oman kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Nyota huyo alijiunga na Wagosi wa Kaya wakati wa dirisha dogo la usajili akitokea FleetWoods Falme za Uarabu, UAE alikocheza kwa misimu miwili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mgaya alisema ameamua kuichagua timu hiyo kutokana na ofa nzuri waliyoweka ingawa hakutaka kuweka wazi kiasi cha dili hilo.
“Kama unavyofahamu nilikuwa na ofa nchi tatu, Kazakhstan, Jordan na Oman, niliamua kubaki hapo kwa sababu tofauti kwanza Uarabuni nimeshacheza najua ligi za huko pili ofa ilikuwa kubwa,” alisema Mgaya na kuongeza
“Sio ligi ngumu sana tofauti na Falme za Kiarabu nilipotoka kabla ya kurejea nyumbani lakini ina ushindani wa aina yake, nimejiandaa vilivyo kukabiliana napo na naamini utakuwa mwanzo mzuri kwangu.”
Chama hilo lililoanzishwa mwaka 1981, lakini awali haikuwekeza zaidi kwenye soka ikiweka nguvu kubwa kwenye mpira wa kikapu, mpira wa mikono, skwashi na michezo mingine.
Kwenye soka iliwekwa kipaumbele cha mwisho kwani tangu ianzishwe haijawahi kunyakua taji lakini ilimaliza nafasi ya pili mara mbili, msimu wa 2009/2010 na 2014/2015.
Akiwa Coastal Union alicheza mechi tatu, Fleetwoods ya Uarabuni alifunga mabao 20 kwenye misimu miwili aliyoitumikia timu hiyo iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la kwanza.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Coastal Union ya vijana hiyo inakuwa timu ya pili kuichezea nje ya Tanzania na zote zikiwa nchi za Kiarabu.