Kongwa. Mgombea ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kongwa, Isaya Mngulumi anafanya kazi na waliokuwa wagombea wenzake ili kutafuta kura.
Kitendo hicho kinatajwa kuwa mkakati wa kumaliza makundi ndani ya chama.
Hata hivyo, aliyeshika nafasi ya tatu katika kura za awali Deus Seif ameonekana kuwa turufu ya chama hicho ndani ya jimbo akitakiwa kusaidia kusaka kura.
Jana Septemba 13,2025 Mngulumi alimsimamisha Deus ili aombe kura katika Kata ya Kibaigwa ambayo ina idadi kubwa ya wapiga kura.
Jimbo la Kongwa lilifanya uchaguzi wa kura za maoni mara mbili baada ya ule wa awali kufutwa kutokana na kifo cha aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge Job Ndugai ambaye kwenye kura hizo aliongoza.
Akihutubia umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo, Deus aliwataka kusimama na Mngulumi kwani uzoefu wake katika utumishi utakuwa mhimili wa kuwapeleka katika malengo tarajiwa.
Dues aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) amewataka wananchi kupiga kura nyingi za kishindo kwa wagombea wa CCM ili waweza kuendelea yale ambayo aliyaanzisha marehemu Job Ndugai.
“Tunadai maendeleo na lazima tuyapate, lakini tutayapata kama tutachagua mafiga matatu kwa wagombea wa CCM ambao Rais, mbunge na diwani,” amesema Deus.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mngulumi amesisitiza uongozi shirikishi akiahidi kufanya kazi ya siasa karibu na Deus.
Mngulumi amesema anatambua uwezo mkubwa alionao mwalimu Deus akisema uwezo wake katika utumishi na kada ya ualimu kwa nafasi waliyopitia, akimtaka asaidie kupeleka maendeleo Wilaya ya Kongwa.
Pia, amesisitiza kupambania maendeleo kwenye sekta ya elimu,afya na miundombinu ili ndoto za wananchi zitimie.
Kwa Kata ya Kibaigwa amewataka wananchi kumpa kura ili afanye mageuzi makubwa na miundombinu katika mji huo unaobeba sura ya kibiashara kwa Wilaya ya Kongwa.