Shigela: Wananchi heshimuni sheria bila shuruti

Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amewataka wananchi kuheshimu vyombo vya dola na kutii maelekezo yake bila shuruti hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza leo Septemba 14,2025,wakati wa kukabidhi magari mapya 15 kwa jeshi la polisi mkoani humo, Shigela amesema ni desturi ya Watanzania kuheshimu askari polisi, hivyo ni vyema kuendeleza utamaduni huo.

Shigela ametoa rai wakati wa hafla ya kukabidhi magari 15 mapya kwa Jeshi la Polisi mkoani humo na kusema nchi imekabidhiwa askari kwa ajili ya kulinda amani na utulivu.

Amefafanua ili askari waweze kutekeleza majukumu yao wamekabidhiwa silaha ili asiyetaka kutii kwa maneno atii kwa shuruti.

Amesema vifaa hivyo havijatolewa kwa ajili ya vitisho au mbwembwe bali ni nyenzo za kulinda raia na mali zao, akisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola ili kudumisha amani na usalama.

“Sisi wanageita na Watanzania kwa jumla tuna utamaduni wa kutii maelekezo ya polisi ni vyema tukauendeleza. Wapo wanaodhani wakati wa uchaguzi jeshi liko likizo, na kutumia uhuru wa kujieleza na mikutano vibaya wakidhani nchi itaendelea kuwa na utulivu,jambo kama hili haliwezi kuvumiliwa na ndio maana serikali inaendelea kuimarisha vyombo vyake,”amesema.

Aidha, Shigela amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani Geita kwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu katika kipindi cha miaka mitatu aliyohudumu kama mkuu wa mkoa.


Amesema awali kulikuwa na malalamiko ya wananchi kuhusu uonevu, wizi wa mifugo,kusingiziwa na vitendo vya rushwa hasa katika shughuli za madini, lakini sasa hali imeimarika na wananchi wanafanya shughuli zao kwa uhuru.

Katika hatua nyingine amewataka askari kuhakikisha wanatunza magari na vifaa walivyokabidhiwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu, huku akiwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka kwa maendeleo ya nchi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema magari yaliyokabidhiwa yatawasaidia askari kufika maeneo yaliyokuwa hayafikiki kwa urahisi na hivyo kuongeza ufanisi wa kazi za kulinda usalama.

Amesema magari hayo yametolewa kwa nyakati tofauti kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, na kugawanywa kwa wakuu wa upelelezi, wilaya na vitengo vya jeshi hilo.