JAMBO GROUP MDHAMINI MKUU PAMBA JIJI FC

Viongozi wa Jambo Group na viiongozi wa Pamba Jiji FC katika picha ya pamoja.


Pamba jiji FC wakitembelea kiwanda cha Jambo Food product.

Na Eunice Kanumba-Shinyanga

Kampuni ya Jambo Group ya mjini Shinyanga sasa ni mdhamini mkuu wa timu ya Pamba FC ya jijini Mwanza katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza rasmi Septemba 16, 2025. Makubaliano ya udhamini huo yamesainiwa leo katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo Kata ya Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza hayo Septemba 13 ,kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jambo Group, Meneja wa Jambo Media na msimamizi wa chapa, Nickson George, amesema hatua hiyo siyo tu udhamini, bali ni ushirikiano wa kibiashara na kijamii utakaosaidia kukuza chapa za pande zote mbili kupitia michezo.

“Leo ni historia ya azimio la pamoja kati ya taasisi yetu na uongozi wa Pamba FC. Mkataba huu una lengo kuu la kukuza chapa zote mbili, hususan bidhaa za Jambo Group,” amesema George.
Viongozi wa Jambo Group na Pamba jiji Fc wakisaini mkataba wa ushirikiano wa chapa za pande mbili.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Pamba FC, Peter Lehlet, amesema udhamini huo ni mwanzo wa ukurasa mpya wa mafanikio kwa klabu hiyo.

Amefafanua kuwa Pamba na Jambo Group walishirikiana awali, wakasitisha kwa muda, lakini sasa wamerejea tena kuendeleza gurudumu la michezo.

Naye Mwenyekiti wa Pamba FC, Bikhu Cotecha, ameishukuru Jambo Group kupitia Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salum Khamis, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, kwa mchango wao kuhakikisha klabu hiyo inaendelea kushiriki Ligi Kuu.
Amesisitiza kuwa historia ya ushirikiano kati ya Pamba na Jambo Group ni ya muda mrefu na yenye matunda.

Kwa upande wa wachezaji, Nahodha wa timu hiyo, James Mwashinga, ameahidi kupambana na kufanya vizuri katika msimu huu ili kuipa heshima chapa ya Jambo Group na mashabiki wa Pamba FC.

Pamba FC inatarajiwa kushuka dimbani Septemba 18, 2025 dhidi ya Namungo FC katika Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi, ikiwa ni mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu.

Kampuni ya Jambo Group imekuwa mdau mkubwa wa soka nchini kwa nyakati tofauti, ikiwahi kudhamini timu mbalimbali za Kanda ya ziwa, ikiwemo Stand United ya Shinyanga.






Wachezaji na viongozi wa pamba fc wakitembelea kiwanda cha Jambo Food product.