ATTF na Arthshakti Foundation Kushirikiana Kutoa Elimu ya Matumizi Sahihi ya Mitandao na Kuendeleza Uchumi Jumuishi

Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv

Taasisi ya Africa’s Think Tank Foundation (ATTF) kwa kushirikiana na Arthshakti Foundation nchini Tanzania imesema itaendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Kwa mujibu wa taasisi hizo, kumekuwapo na ongezeko la matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ambapo watu huandaa na kusambaza taarifa bila kuzingatia madhara ya baadaye.

Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo yaliyofanyika Septemba 13, 2025 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa ATTF, Elizabeth Riziki amesema Tanzania siku zote ni nchi ya amani na utulivu.

“Watu wengi hutumika na wanasiasa kuchafua wenzao mitandaoni badala ya kutumia mitandao kujipatia kipato. Ndiyo maana tumeingia makubaliano haya ili kutoa elimu kwa rika zote, tukisisitiza matumizi ya mitandao kwa manufaa ya kifedha na kukuza uchumi,” amesema Riziki.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha uchaguzi watu hutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha ushindi, lakini mara nyingi husahau kuwa Tanzania ni “kisiwa cha amani” kinachothamini utu na mitazamo ya kila mtu. Nakusisitiza kwamba matumizi sahihi ya mitandao yatasaidia pia kupunguza matapeli mtandaoni.

Akielezea ushirikiano huo, Elizabeth amesema hatua hiyo ni ya kihistoria kwa kuwa inalenga kuimarisha uchumi jumuishi, uwezeshaji wa jamii, uimara wa kidijiti na kilimo endelevu nchini Tanzania na barani Afrika.

“Ushirikiano huu si mkataba pekee wa taasisi mbili, bali ni ahadi ya pamoja kubadilisha maisha kupitia kuimarisha uwezo wa wakulima wadogo, kuwajengea jamii elimu na maarifa ya kifedha, na kujenga mustakabali ambapo teknolojia na maendeleo endelevu vinashirikiana,” amesema.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, programu zitakazotekelezwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya elimu kupitia kuanzisha maktaba za kidijiti mashuleni,kusongesha mbele elimu ya kidijiti na uelewa wa usalama mtandaoni (cyber-smart awareness),kuimarisha utunzaji wa mazingira, ikiwemo kudhibiti taka za kielektroniki na matumizi bora ya maji,kuwezesha jamii kwa elimu ya kifedha, ujasiriamali wa vijana na uwekezaji pamoja na kukuza tafiti na bunifu za sera zinazohusiana na vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania na Afrika.

Elizabeth amebainisha kuwa ATTF italeta utaalamu katika ubunifu wa sera, utawala bora na mageuzi ya kidijiti, huku Arthshakti Foundation ikiongoza miradi yenye mwelekeo kwa wakulima na jamii.

Aidha, ametoa wito kwa serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizo kwa manufaa ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ushirikiano na Ubia wa Kimkakati wa ATTF, Alfred Tembo, amesema watu wengi huathirika kisaikolojia na kijamii kutokana na taarifa zao binafsi kuvuja mitandaoni, jambo linalosababisha wengine hata kupoteza maisha. Amesisitiza umuhimu wa kulinda masilahi binafsi.

Naye Mwakilishi wa Arthshakti Foundation, Mira Solanki amesema Tanzania ni nchi ya demokrasia, na kupitia ushirikiano huo watatoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya pembejeo bora pamoja na kufanya tafiti za udongo ili kuboresha kilimo.

“Changamoto kubwa ya kilimo siyo udongo pekee bali ni elimu duni. Wakulima wengi hutegemea mvua na kilimo cha mazoea bila kujua mahitaji halisi ya udongo wao. Kupitia ushirikiano huu tutawapa elimu, huduma za kifedha, afya na hata vifaa ikiwemo matrekta ili kukuza kilimo endelevu,” amesema Solanki.