Sumaye asema Samia amedumisha amani, utulivu nchini

Mwanga/Same. Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Frederick Sumaye amesema miaka minne ya utawala wa Samia Suluhu Hassan umedhihirisha uimara wake wa kudumisha amani na utulivu nchini na kurudisha uhusiano wa kidiplomasia duniani.

Wakati Sumaye akieleza hayo, mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema Samia anaishi kiapo alichokiapa cha kuilinda Katiba.

Sumaye na Dk Nchimbi wamesema hayo leo Jumapili, Septemba 14, 2025 katika mikutano ya kampeni iliyofanyika majimbo ya  Mwanga na Same Magharibi, mkoani Kilimanjaro.

Mikutano ya Dk Nchimbi ilianza Agosti 29, 2025 jijini Mwanza kisha ikaendelea Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera, Rukwa, Katavi, Arusha na sasa yupo Kilimanjaro.

Rais Samia alianza Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa, Singida, Tabora na amemalizia Kigoma leo Jumapili kisha atakwenda Zanzibar.

Katika mikutano ya leo Jumapili, Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu 1995 hadi 2005 na Dk Nchimbi wamezungumzia mafanikio ya utawala wa Samia na kipi kinakwenda kufanyika miaka mitano ijayo.

Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Samia ni miongoni mwa wagombea 18 wa urais wanaosaka kuwaongoza Watanzania takribani milioni 61.

Kampeni za uchaguzi huo, zilianza Agosti 28 na zitahitimishwa Oktoba 28, 2025. Upigaji kura utakuwa Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Katika mkutano uliofanyikia Uwanja wa Stesheni, Same na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi na wanachama, Sumaye amesema Samia ni kiongozi mwenye upeo mkubwa anayetamani kuiona:”Nchi iko kwenye barabara nzuri ya uelekeo mzuri.”

Sumaye ambaye ni mratibu wa kampeni za CCM, mikoa ya kaskazini amesema ndiyo maana ameanzisha na kupatikana Dira ya Maendeleo 2050 ambayo utekelezaji wake utaanza akiwa madarakani na ataiacha nchi ikiwa na uelekeo unaoeleweka wenye tija.

“Mama Samia tangu alipoingia madarakani miaka minne na nusu, amefanya mambo makubwa na kubwa zaidi ni nchi imetulia, wale waliokuwa na chokochoko nyingi, Mama Samia alileta 4R na katika hizo R moja ni maridhiano.”

Huyu mama ni bingwa wa demokrasia na alipokuwa anaapishwa aliapa kuilinda Katiba kwamba nchi hii ni ya vyama vingi vya kidemokrasia,” amesema Sumaye.

Amesema aliwaita wapinzani na kuzungumza nao ili kujua tatizo lililopo na kubwa ambalo Samia alisisitiza anahitaji kuongoza nchi yenye umoja.

“Akiona kuna mahali kunafukuta, anawaita, mnazungumza na nchi imetulia. Hakuna mtu kama huyu,” amesema Sumaye.

Kiongozi huyo mstaafu, amesema wakati anaingia madarakani, diplomasia ya kimataifa ya Tanzania:”Hatukuwa wazuri sana, mara tumekosea hapa, mara hivi, lakini alipoingia alirekebisba vikasoro vyote na leo diplomasia ipo juu sana na Mama Samia anahesimika na ameiletea heshima kubwa nchi yetu.”

“Siyo majirani zetu, Afrika tu bali dunia nzima. Sasa Mama Samia ndiyo mgombea wetu wa urais, hebu niambieni kwa haya aliyoyafanya nani hatamchagua.”

Awali, kwenye mkutano uliofanyika Uwanja wa Cleopa Msuya, Jimbo la Mwanga, Sumaye amesema hakuna namna ambayo Samia anaweza kuendelea kuwa Rais kama wananchi hawatajitokeza kumpigia kura kura.

Amesema hiki ni kipindi cha kila aliyejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kukiandaa kitambulisho chake (huku akikitoa chake na kuwaonesha) ili siku ikifika wasije kukikosa wakakosa fursa ya kwenda kuwachagua viongozi wa CCM.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Namelok Sokoine amesema chama hicho kimewapeleka wagombea wazuri kwa wananchi, wanaochagulika na watakaosikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi.

“Wagombea hao yupo Samia, Dk Nchimbi, mgombea wetu wa ubunge wa Mwanga, Dk Magembe na madiwani. Kikubwa nawaomba mjitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura na kura tutapiga tatu na zote kwa CCM,” amesema Namelok ambaye ni mtoto wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward Sokoine.

Katika mikutano hiyo miwili, Dk Nchimbi pamoja na kueleza mafanikio makubwa kwenye sekta za afya, elimu, miundombinu, nishati ya umeme, kilimo, ufugaji na utalii amegusia utendaji wa  Samia.

Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya uongozi wa Samia ambaye aliapa:”Kulinda Katiba, kulinda amani, aliapa kupeleka  maendeleo bila ubaguzi,

aliapa kulipa mipaka ya nchi na kazi hiyo ameifanya kwa kiwango kikubwa  na kulinda kiapo chake. Kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi tunampongeza sana.”

“Kwa hiyo…. amejielekeza katika mahitaji ya wananchi wake, ameelekeza nguvu kwenye afya, elimu za watoto wetu. Ameelekeza nguvu kwa wakulima na ufugaji.

“Kwa hiyo tunaweza kusema pasipo shaka kwamba amemudu jukumu alilopewa na tunasema tumpe mitano mingine ili aweze kutuongoza tena,” amesema Dk Nchimbi.

Mgombea mwenza huyo, amesema:”Nchi yetu ni huru, ina mshikamano na inapiga hatua kila mahali, hakuna mkoa, wilaya, kata, kijiji, kitongoji au mtaa haujafikiwa na maendeleo. (Samia) amejielekeza kwenye mambo ya msingi kama elimu, afya, miundombinu, kilimo, ufugaji, changamoto zote za msingi za kukuza uchumi wa nchi yetu.”

Kuhusu maji, Dk Nchimbi amempongeza Samia kwa kuusimamia ipasavyo na kuuzindua mradi wa maji Mwanga- Same- Korogwe wa zaidi ya Sh300 bilioni ambao umepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya maji ktika maeneo hayo.

“Mradi ambao ulikuwa umekatiwa tamaa, yeye akasema nitautekeleza, mateso wanaopata kina mama na ndiyo maana miradi inayohusu kina mama inapewa kipaumbele kama afya akijuwa ndiyo waathirika wakubwa,” amesema.

Amesema, miaka mitano iliyopita, wilaya ya Same mabwawa ya samaki yameongezeka kutoka 80 hadi 100.

Zahanati zilikuwa 36 sasa zipo 56.

Gari za kubeba wagonjwa zimefika 15 kutoka 10. Shule za msingi, sekondari mpya zimejengwa sawia na madarasa.

Amesema Serikali ya CCM, miaka mitano ijayo wilayani Mwanga inatarajia kuongeza mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami ikiwemo barabara ya Msuya kilomita 13, kujenga stendi ya mabasi eneo la Mwanga ambayo itakuwa na maduka mazuri ya kisasa.

Dk Nchimbi ameahidi kuanzishwa mashamba darasa ya uvuvi ili watu wajifunze mbinu mbalimbali za kilimo.

Kuhusu umeme Mwanga, vijiji vyote vina umeme huku vitongoji vitano pekee kati ya 282 ndiyo havijafikiwa na kuahidi kwenda kuunganishiwa huduma hiyo iwapo wataichagua CCM.

Mbunge wa zamani wa Busega, Mkoa wa Simiyu, Dk Raphael Chegeni akizungumza kwenye mkutano wawanga amesema Samia ameleta maendeleo na mageuzi ya kiuchumi mkoa wa Kilimanjaro, “na kama ameleta haya wewe ni nani hutaki kumpa kura Samia.”

“Nchi yetu sasa hivi ina amani na utulivu, Samia tumempa kazi kubwa sana na ameifanya vizuri na ameamua kumtafuta msaidizi wake Dk Nchimbi aliyetokana na chama. Twendeni tukawachague kwa kura nyingi,” amesema Dk Chegeni.

Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Wilaya ya Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma, Hamis Ally amesema hakuna njia nyingine ya kumfanya Samia awe Rais wa Tanzania zaidi ya kura.

“… amefanya mambo mengi na makubwa. Kila mmoja anaona, njia pekee ya kumfanya aendelee kubaki madarakani kututumikia, tujitokeze kwa wingi sana Oktoba 29 kupiga kura na kura nyingi za kishindo,” amesema Ally.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua yanayokea kwenye mikutano ya kampeni ya Dk Nchimbi