Tabora. Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa kwenye ajali ya moto katika eneo la Ikindwa, kata ya Mapambano, manispaa ya Tabora.
Tukio hilo lilitokea asubuhi ya Septemba 13, 2025, ndani ya chumba wanacholala watoto hao, na mmoja kati yao alikuwa akichezea kiberiti na kisha kuwasha moto ulioshika kwenye godoro na kuwateketeza.
Akizungumza kwa njia ya simu leo Septemba 14, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa watoto waliofariki dunia kuwa ni Jefta Hilari (6) na Eliana Hilari (4).
Amemtaja aliyejeruhiwa kuwa Osnili Hilari (7), anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Jeshi ya Milambo kutokana na majeraha yaliyosababishwa na moto huo.
“Mmoja wa watoto hawa alikuwa akichezea kiberiti chumbani kwao. Wakati akiwasha, njiti ya moto ikagusa godoro na moto ukashika. Bahati mbaya, watoto hao walikuwa ndani peke yao, huku mama yao akiwa ameenda kanisani,” amesema kamanda.
Amesema mbali na kusababisha vifo na majeruhi, moto huo umeteketeza vitu vyote vilivyokuwa ndani ya chumba hicho.
“Mama wa watoto hawa, usiku wa kuamkia siku ya tukio, alienda kanisani kwenye mkesha, na aliwafungia mlango watoto wake wakiwa peke yao. Hivyo, akiwa kanisani alipopokea taarifa za tukio, watoto tayari walikuwa wamepata majeraha makubwa,” ameongeza kamanda.
Aidha, shuhuda wa tukio hilo, ambaye ni bodaboda katika eneo hilo, Ramadhani Ibrahim, amesema: “Nilisikia kelele, na nilipofika eneo la tukio nikakuta moto ukiwa umeshateketeza chumba hicho.
“Tukashirikiana na watu wengine kuwatoa watoto na kuwapeleka hospitali. Mtu mzima kidogo alikuwa anakimbia hovyo, nikamchukua kwenye pikipiki yangu, wengine wakapanda kwenye gari, na wale watoto wote tukawaelekea Hospitali ya Milambo. Baada ya muda mfupi tukaambiwa watoto wawili wameshafariki, ila yule mmoja bado anapata matibabu.”
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Dayosisi ya Magharibi, Tabora, mtaa wa Ikindwa, Moses William, amewahimiza waumini na hasa familia kuwa watulivu wakati wa changamoto hiyo, akisema ni fumbo la imani.
“Mungu ana mpango mkuu kwa familia hii pamoja na jamii kwa ujumla, hivyo ni vyema kuwa watulivu wakati wote,” amesema mchungaji.