Moshi. Mgombea udiwani wa Njoro, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Zuberi Kidumo amewaomba wananchi kumpa ridhaa nyingine ya kuongoza kata hiyo ili aweze kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa, ikiwamo ya barabara na ujenzi wa Zahanati ya Njoro.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Reli, Kidumo amesema kwa kipindi cha miaka mitano aliyohudumu kama diwani, kata hiyo imenufaika na maendeleo makubwa kwenye sekta za barabara, afya, elimu na michezo.
“Nimekuwa diwani wenu kwa miaka mitano.
Wananchi mnatambua tuliyoyafanya, ikiwamo kuboresha barabara na kwa sasa Barabara ya Pepsi, ambayo kwa muda mrefu imekuwa changamoto, inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami,” amesema Kidumo.
Amefafanua kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake ni kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Njoro na kusimamia upatikanaji wa vifaa tiba.

Mgombea udiwani wa viti maalum Manispaa ya Moshi, Hilda Mjema
“Wodi ya kisasa ya kina mama tayari imekamilika kwa msaada wa wadau, na vifaa tiba vitawasili muda wowote. lakini pia tuna mpango wa kujenga wodi nyingine pale,nia yetu ni kuwekeza zaidi kwa mama na mtoto katika eneo hilo na kuhakikisha wanapata huduma zote muhimu wanapofika katika zahanati hiyo,” amesema Kidumo.
Mbali na afya, Kidumo ameahidi kusimamia upanuzi wa Soko la Njoro na kulifanya la kisasa ili kuimarisha mazingira ya biashara.
“Tutapanua soko letu la Njoro na kulifanya kuwa la kisasa, lakini pia baada ya baraza la madiwani kuanza tutaomba kupanga bidhaa kwa masoko maalumu, yaani kila soko liwe na bidhaa ya tofauti ambayo itavuta wateja na lengo letu ni kukuza uchumi wa wananchi na kuongeza kipato,” ameongeza.
Kadhalika, amesema ataendelea kusimamia mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ili kuwezesha makundi hayo kujikita katika shughuli za kiuchumi.
Kidumo amewataka wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuondoa tofauti za kisiasa zilizojitokeza wakati wa kura za maoni na kushirikiana kuhakikisha ushindi wa chama hicho.
“Tunataka Njoro iwe kinara wa kura nyingi kwa CCM. Tumchague Samia (Suluhu Hassan), Mbunge Ibrahim Shayo na mimi Zuberi Kidumo kuwa diwani, ili tuendelee na miradi ya maendeleo,” amesema.

Mgombea udiwani wa viti maalumu Manispaa ya Moahi, kupitia CCM, Hilda Mjema amewataka wanachama kushirikiana kuhakikisha chama hicho kinashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu.
Amesema utekelezaji wa ilani ya CCM 2020/25 umefanyika kwa mafanikio makubwa.